Katibu Mkuu Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi akizungumza kuhusiana na Mashindano ya Umiseta |
MSANII Chege Chigunda ambaye ni miongoni mwa Wasanii watakaotumbuiza wakati wa Ufunguzi wa MAshindano ya UMISSETA
Na John Mapepele, Mtwara
Wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya, wakiongozwa na Maua Sama na Chegi wanatarajia kupamba ufunguzi wa Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yatakayofunguliwa kesho Juni 21, 2021 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Profesa Joyce Ndalichako (Mb) kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza kikamilifu na inaendelea kutoa kipaombele kwenye Sekta ya Sanaa hivyo anawaalika wadau mbalimbali kuja kushuhudia burudani mwanana zinazoendelea kwenye mashindano haya kutoka kwa wasanii wenye vipaji wanaokuja juu hapa nchini.
Amesema wakati wa ufunguzi wa UMITASHUMTA wasanii mbalimbali wakiongozwa na Ibrah kutoka Konde Gang,Beka Flavour, Peter Msechu na Linah Sanga, pia msanii maarufu wa Singeli Dulla Makabila na Mfalme wa taarabu Mzee Yusuf, walitoa burudani ambapo amesema katika awamu hii vikundi mbalimbali vya ngoma za asili, kwaya na Sanaa nyingine vimealikwa ili kuongeza hamasa na kutoa burudani wakati mashindano hayo yanaendelea.
Aidha, amesema kwenye mashindano hayo Serikali imealika vilabu, vyama, na mashirikisho mbalimbali kuona vipawa na vipaji vya wanamichezo hao chipukizi kutoka Tanzania Bara na visiwani ili waweze kuwaendeza.
Dkt.Abbasi amesisitiza kuwa mashindano haya yataendelea kutumbuizwa na wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Mtwara, ambapo burudani pia kutoka vikundi vya ngoma za asili, kwaya na Sanaa nyingine vitaonesha umahiri wao.
“Hii ni kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Serikali inakuja na kitu cha tofauti kabisa kwenye mashindano haya wasanii wametumbuiza, michezo na fani ya sanaa za ndani zimeshiriki kikamilifu kwa mikoa yote” ameongeza Dkt. Abbasi
Ameitaja michezo itakayoshindaniwa katika mashindano haya ni mpira wa miguu kwa wasichana na wavulana, mpira wa miguu maalum kwa wavulana (wenye ulemavu wa kusikia) mpira wa pete, mpira wa wavu kwa wasichana na wavulana, mpira wa mikono kwa wasichana na wavulana, mpira wa kikapu kwa wasichana na wavulana, mpira wa meza kwa wasichana na wavulana, riadha jumuishi, kwaya na ngoma.
Amewataka wazazi kuondokana na fikra potofu ya kwamba michezo na sanaa ni uhuni badala yake wawahimize Watoto kushiriki kikamilifu katika michezo kwa kuwa kiuna uhusiano mkiubwa kati ya taaluma na michezo.
Amesema kauli mbiu ya mwaka huu ambayo inasema “Michezo, Sanaa na Taaluma kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda” inaelezea uhusiano na nafasi kubwa iliyopo ya Michezo, Sanaa na Taaluma katika ujenzi wa uchumi wa Taifa hivyo amewataka waratibu wa kila mchezo kuzingatia sheria na taratibu za michezo husika ili kuwapata washindi bora ili waweze kufika mbali zaidi kwenye michezo yao.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipa michezo na sanaa kipaombele na kuwataka waratibu na wanamichezo wote kwenye mashindano haya kuchukulia michezo hii kama msingi wa mapinduzi makubwa kwenye sekta hizo hivyo kushiriki kwa weledi zaidi.
Mashindano yameandaliwa na Wizara tatu zinazohusika na Elimu, Michezo na TAMISEMI chini ya Kamati ya Uratibu ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu wa Wizara hizo.
Mashindano haya yalitanguliwa na Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) yaliyofunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa Juni 8, mwaka huu mjini Mtwara na kufungwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Pauline Gekul Juni 18, 2021.Mashindano ya UMISSETA yanatarajiwa kufungwa rasmi Julai 3, mwaka huu.
Social Plugin