NA MWANDISHI WETU
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata amezungumza na viongozi wa wafanyabiashara wa wilayani Kasulu na Kigoma ambapo ameambatana na baadhi ya viongozi waandamizi kutoka TRA Makao Makuu akiwemo Kamishna wa Kodi za Ndani Bw. Hebert Kabyemela, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo na Naibu Kamishna wa Walipakodi Wakubwa Bw. Beatus Nchota.
Pamoja na viongozi hao waandamizi, Kamishna Mkuu Bw. Kidata amekwenda na timu ya watalaam wa kutoa elimu na huduma kwa mlipakodi kwa lengo la kutatua changamoto zilizojitokeza wilayani humo na kuhakikisha wanapita kila duka yaani mlango kwa mlango kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu sheria na taratibu za ulipaji kodi.
Akizungumza na viongozi hao wa wafanyabishara katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Kamishna Mkuu Kidata alisema kuwa, timu hiyo ya watalaam wa elimu kwa mlipakodi watakaa wilayani humo kwa wiki nzima wakipita duka kwa duka wakitoa elimu ya kodi na kutatua haraka changamoto za kikodi zinazowakabili wafanyabiashara hususani makadirio ya kodi.
“Ndugu zangu nimepokea maoni, ushauri na changamoto zenu na mimi kwa kulitambua hili nimekuja na timu ya watalaam kutoka TRA Makao Makuu ambao nitawaacha hapa kwa ajili ya kuwaelimisha sheria na taratibu za ulipaji kodi ikiwa ni pamoja na haki na wajibu wenu. Pia, watamsikiliza kila mfanyabiashara mwenye changamoto na kuzitatua,” alisema Bw. Kidata.
Kamishna Mkuu Kidata aliwaambia viongozi hao kwamba, ni muhimu kila upande yaani wafanyabiashara na watumishi wa TRA kuzingatia haki na wajibu wao kila wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
“Sisi watumishi wa TRA tunafanya kazi kwa kufuata misingi yetu ya maadili ambayo ni uwajibikaji, uadilifu na weledi lakini pia kama mmoja wenu alivyosema, ni lazima pia sote, ninyi na sisi TRA tuzingatie haki na wajibu kila tunapotekeleza majukumu yetu,” alisema.
Kwa upande wa viongozi hao, walisema wamefurahishwa na kitendo cha Kamishna Mkuu wa TRA kufika wilayani hapo na kufanya nao mazungumzo pamoja na kupeleka timu ya watalaam kutoa elimu kwa walipakodi hao kwa lengo la kutatua changamoto zilizojitokeza baina ya wafanyabiashara wa wilayani Kasulu na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
“Ndugu Kamishna Mkuu, tunakushukuru sana kwa kuja kuzungumza na sisi na tumefurahi sana kwa kutuletea watalaam wa kutuelimisha na kutatua changamoto za mfanyabiashara mmoja mmoja kama zilivyowasilishwa kwako leo,” alisema Bw. Prosper Guga ambaye ni Katibu wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) wilayani Kasulu.
Kabla ya kuzungumza na viongozi hao wa wafanyabiashara wa Kasulu, Kamishna Mkuu Bw. Alphayo Kidata alipata nafasi ya kuwatembelea baadhi ya viongozi wa serikali mkoani Kigoma ambapo alifanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe. Samson Anga na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mhe. Kanali Simon Anange.
Aidha, Kamishna Mkuu huyo alipata fursa ya kuzungumza na watumishi wa TRA wa Mkoa wa Kigoma na kuwataka kuzingatia kufanya kazi kwa bidii na weledi ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati na hiari huku wakiwapatia elimu ya kodi.
Hivi karibuni, wafanyabiashara wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma walifanya mgomo wa kufunga maduka wakidai kuwa watumishi wa TRA wilayani humo hawana lugha nzuri na wanawakadiria makadirio makubwa suala linalowapelekea kushindwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, kutokana na mazungumzo yaliyofanyika baina ya viongozi mbalimbali wa serikali na wafanyabiashara hao, tayari maduka yamefunguliwa na shughuli za kibiashara zinaendelea kama kawaida.