Na Munir Shemweta, WANMM MVOMERO
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameagiza kufanyika upekuzi wa mashamba 86 yasiyoendelezwa katika wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro ili yatakayobainika kutoendelezwa, mapendekezo ya kufutwa yapelekwe kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani.
Waziri Lukuvi alitoa agizo hilo leo tarehe 8 Juni 2021 wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na viongozi, watendaji wa kata za wilaya ya Mvomero na wananchi wa Wami Dakawa akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani Morogoro.
Alisema, katika wilaya ya Mvomero kuna mashamba 86 ambayo uendelezaji wake una mashaka hivyo ni vizuri ukafanyika upekuzi haraka na yale yasiyokidhi vigezo wamiliki wake wapewe notisi za ufutaji na kusisitiza kuwa serikali haitaacha kuchukua hatua kwa mashamba yasiyoendelezwa.
" Ningefurahi katika kipindi cha miezi miwili ya sita na saba 2021 kazi ya upekuzi mashamba hayo iwe imefanyika ili kupunguza migogoro ya ardhi kati ya wamiliki na wananchi na lazima hatua zichukuliwe" alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, kazi ya upekuzi mashamba ni ya msingi na waliopewa mashamba wafahamu kuwa walipewa mashamba ili kuyaendeleza na sheria inataka mmiliki wake walau awe ameendeleza moja ya nane ya shamba zima kwa mwaka mmoja.
"Tatizo la Mvomero ardhi imechukuliwa na wamiliki wake wamefungia hati bila kulipa kodi wala kuendelezwa na upekuzi huu unaofanyika ni kutaka kujua kila halj ya shamba" alisema Lukuvi
Naye Mbunge wa Jimbo la Mvomero Jonas Van-zeland alisema, wilaya Mvomero inayo migogoro mingi ya ardhi ikiwemo utelekezaji mashamba jambo alilolieleza kuwa limechangia wananchi kushindwa kufanya shughuli za kijamii na kuongeza kuwa wamiliki wa mashamba hayo wengi hawajulikani na wananchi.
Aidha, Waziri Lukuvi katika ziara yake wilayani Mvomero alisema, wilaya hiyo imekuwa na migogoro mingi ya ardhi ikiwemo ile ya mipaka ya vijiji na wilaya na kubainisha kuwa jukumu la kutafuta suluhu ya migogoro ya mipaka ni la viongozi wa mkoa na wilaya.
" Why migogoro ya mipaka inaendelea wakati wilaya na mkoa ipo na mipaka iliyopo ni ya kiutawala na isiwe kikwazo cha shughuli za wananchi na mtu asizuiwe kuchunga nje ya mipaka ya kiutawala cha msingi pawepo utaratibu" Waziri Lukuvi.
Katika hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Sukuhu Hassan ameendelea kushusha neema kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro ambapo safari hii amefuta jumla ya mashamba 9 yenye ukubwa wa ekari 13,900.5 katika halmashauri ya wilaya ya Mvomero na kuelekeza sehemu kubwa ya mashamba itumike kutatua shida za wananchi.
Waziri Lukuvi alisema kati ya ekari zilizofutwa ekari 9,700 zigawiwe kwa wananchi kwa ajili ya matumizi mbalimbali na ekari 4,100 zitengwe kwa ajili ya shughuli za uwejezaji na kusisitiza watakaopewa hawatakiwi kuyauza.
" Rais amesisitiza kila eneo lililofutwa basi kipaumbele kiwe kwa wananchi ambao hawana ardhi hasa vijana wasiowahi kuwa na ardhi ama zile kaya zisizomiliki ardhi" alisema Lukuvi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shighela kwa upande wake mbali na kumshukuru Lukuvi kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha miaka mitano katika sekta ya ardhi ameweka wazi kuwa utatuzi wa migogoro ya ardhi anaoufanywa na Waziri Lukuvi haulengi mtu mmoja mmoja bali unawalenga walio wengi na kusema kuwa huo ni utekelezaji wa sera ya Chama cha Mapinduzi.
Ametaka kuwepo ushirikiano kati ya uongozi wa mkoa na wananchi wa Mvomero katika kutekeleza maekekezo ya serikali na kutafuta ufumbuzi wa matatizo mengine yasiyohusiana na sekta ya ardhi.
Social Plugin