MAJALIWA: TUMEPUNGUZA SIKU ZA KUSHUGHULIKIA MAOMBI YA VIBALI
الأربعاء, يونيو 30, 2021
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema utaratibu wa utoaji wa vibali vya ukaazi kwa kutumia mfumo wa kielektroniki umesaidia kupunguza hatua za kuchakata maombi kutoka siku 33 za hadi saba.
Amesema kuwa kwa sasa waombaji hawalazimiki kwenda katika Ofisi za Kazi kwa sababu taarifa zote zinapatikana kwenye mfumo na watajaza fomu moja tu ambayo huwa na taarifa zote za kazi na ukaazi tofauti na awali ambapo wawekezaji walilazimika kujaza fomu mbili.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 30, 2021) wakati akiahirisha mkutano wa tatu wa Bunge la 12, Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Agosti 31 mwaka huu.
Amesema miongoni mwa manufaa yaliyopatikana kupitia matumizi ya mfumo huo ni kupungua kwa siku za kushughulikia maombi ya vibali vya kazi kutoka siku 14 hadi siku tatu. “Hali hii, pamoja na mambo mengine, imesaidia kupunguza malalamiko ya kuchelewa kupata majibu ya maombi ya vibali vya kazi.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kupokea maoni kutoka kwa watumiaji wa mfumo kwa ajili ya maboresho na tayari imeshakutana na kupokea maoni ya wadau wa ndani na nje kikiwemo Chama cha Wafanyakazi, Chama cha Waajiri (ATE), Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Taasisi ya Sekta Binafsi na kuyajumuisha maoni hayo kwenye maboresho.
Amesema Serikali inakamilisha maboresho ya Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni (Sura 436) kwa kuainisha maeneo yaliyokuwa na changamoto za kiutendaji na kuathiri jitihada za kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini. Mfumo huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Agosti mwaka huu.
“Sambamba na marekebisho hayo ya sharia, tangu tarehe 23 Aprili, 2021 tumeanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia maombi ya vibali vya kazi kwa raia wa kigeni na katika hatua za majaribio tayari maombi zaidi ya 500 yameshughulikiwa kupitia mfumo huo.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema ili kuhakikisha bajeti ya 2021/2022 inatoa matokeo yaliyokusudiwa, Serikali itaimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki kwa ajili ya kuongeza uwazi na uwajibikaji na hivyo kudhibiti matumizi ya fedha za umma kwa kuepuka malipo hewa na manunuzi ya umma ya bidhaa na huduma zisizokidhi viwango vya ubora.
Amesema Serikali itahakikisha uwepo wa thamani halisi ya matumizi ya fedha za umma katika utekelezaji wa miradi ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua stahiki tena kwa wakati pale inapobaini ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za umma.
“Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/2022 unakwenda sambamba na Mikakati ya Serikali katika kuimarisha udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, utendaji na uwajibikaji kwa viongozi na watendaji wote wa sekta ya umma. Hatua hizo, zinalenga kuhakikisha bajeti hii inatoa matokeo yaliyokusudiwa.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza watendaji wa Serikali hususan wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wajipange vema na wahakikishe suala la posho za madaraka kwa watendaji wa kata na vijiji kupitia mpango wa halmashauri linasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wahakikishe wanatenga maeneo maalumu kwa ajili ya vijana na wafanyabiashara wadogo sambamba na kuwapatia elimu pamoja na kuwashirikisha katika kubaini maeneo yanayoendana na biashara zao. Amewaagiza watendaji hao wasikilize na kushughulikia kero za wananchi kwa wakati ikiwa ni pamoja na kutenga siku maalum kwa ajili hiyo.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin