Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAJALIWA: WIZARA KILIMO SIMAMIENI KILIMO CHA NGANO NA ZABIBU


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo isimamie upatikanaji wa mbegu bora katika kilimo cha ngano na zabibu pamoja na kuweka mpango mzuri utakaosimamia na kuendeleza kilimo cha mazao hayo .

 “…Utoaji wa vibali kwa wanunuzi wa ngano na mchuzi wa zabibu ufanywe kwa kuzingatia wale ambao watathibitisha kununua malighafi hizo ndani kwanza. Hakikisheni mnasimamia vizuri makubaliano kati ya wakulima na wanunuzi wakubwa ili tusinunue bidhaa hizo kutoka nje.”

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 30, 2021) wakati akiahirisha mkutano wa tatu wa Bunge la 12, Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Agosti 31 mwaka huu.

Akizungumzia kuhusu fursa mpya ya kilimo cha soya, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe inakuwa na mpango mzuri wa kuendeleza kilimo hicho kwa kuwapatia wakulima mbegu kwa kuanza na mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Kadhalika, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu masoko ya mazao ambapo kwa upande wa tumbaku, ameiagiza Wizara ya Kilimo ishirikiane na Wizara ya Fedha na Mipango kukamilisha mazungumzo na wanunuzi wa zao hilo hususan kipindi hiki ambacho bei yake inaonekana kuimarika kwenye soko la dunia.

“Pia nafahamu kuwa tayari tupo kwenye msimu wa pamba. Ninasisitiza kuwa wakulima wa pamba wasikatwe gharama za pembejeo kwa kuwa tayari zipo kwenye mjengeko wa bei. Kwa hiyo, nitoe wito kwa wakulima kupeleka sasa pamba yao kwenye minada ili waweze kunufaika na bei ya sasa.”

Kuhusu kilimo cha mkataba, Waziri Mkuu amesema wameamua kutumia utaratibu huo kwa baadhi ya mazao yakiwemo ya alizeti, ngano, shayiri na soya ili kumpatia tija mkulima, ambapo kwa upande wa soya soko la uhakika lipo nchini China.

“Kwa msingi huo, nasisitiza kwamba Wizara ya Kilimo hakikisheni mikataba inayoingiwa na wakulima inakuwa wazi ikionesha bei na kiwango cha kuuza. Vilevile, simamieni mikataba baina ya wakulima na wanunuzi wakubwa.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara ya Kilimo kwa wazo lao la kuwa na maghala kwenye nchi zenye fursa ya masoko. “Wafuateni wateja msisubiri waje kwenu kwani biashara ni ushindani.”

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com