Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Makamu Wa Rais Aiagiza Wizara Kuangalia Upya Masharti Kuasili Wa Mtoto


Na Mwandishi Wetu Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Philip Mpango ameishauri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, kupitia upya masharti ya utaratibu  wa kuasili watoto  ili kuhamasisha watanzania na watu wengine wenye nia njema  kuasili watoto hivyo kupunguza idadi ya watoto kwenye makao.

Akizungumza June 16, 2021 wakati wa uzinduzi wa Makao ya Taifa ya watoto katika eneo la Kikombo Jijini Dodoma, Makamu wa Rais ameiomba Wizara hiyo kupitia upya utaratibu huo ili kuwapa nafasi watanzania kuasili watoto ambao wanaishi kwenye makao hayo.

"Naomba kutumia fura hii kuishauri Wizara kupitia upya masharti ya utaratibu wa kuasili watoto ili kuhamasisha watanzania na watu wengine wenye nia njema kuasili watoto hivyo kupunguza idadi ya watoto kwenye makao,"amesema Dkt. Mpango.

Hata hivyo, Dkt.Mpango amewasihi watanzania wenye uwezo kuguswa na maisha ya watoto wanaishi kwenye mazingira hatarishi na wachukue hatua kuasili watoto na kuwatunza kwa upendo kwa mujibu wa mila na tamaduni hususani pale inapotokea watoto wa ndugu kufiwa na wazazi.

Vilevile, amewashukuru viongozi wa dini  kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kufundisha na kusimamia maadili mema katika jamii huku akisisitiza viongozi hao kuendelea kulifanya suala hilo kama agenda ya kudumu katika nyumba za ibada  na katika mikusanyiko ya kidini.

"Nawapongeza wasimamizi wote wa vituo  vya kutunza watoto kwa moyo wao wa kujitolea wa kuwalea watoto wetu.Serikali inatambua mchango wenu  katika malezi ya watoto wetu  na naomba kuwatia moyo  muendelee na jukumu hili na Mwenyezimungu atawabariki,"amesema.

Awali Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia,Wazee na Watoto Dkt ,Dorothy Gwajima amesema Juni 16 ni siku ya mtoto wa Afrika ambapo nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika ikiwemo Tanzania wanaadhimisha siku hiyo.

Amebainisha kwamba kama sehemu ya maadhimisho hayo serikali imezindua Makao ya watoto ya Kikombo Mkoani Dodoma ambapo ameitaka jamii kufanya tathmini ni sababu ipi inayopelekea watoto wa mitaani kuongezeka.

Hata hivyo amesema Ujenzi wa Makao hayo unatarajia kuwezesha serikali kutatua changamoto za huduma katika Makao ya watoto kwani kituo cha Kurasini ni kidogo.
Hata hivyo ameeleza kuwa , Ujenzi wa Makao ya Taifa hayo ya watoto yamegharimu Jumla ya  Dola za Kimarekani milioni 5.5 Sawa Shilingi bilioni 12.7 za kitanzania ambapo mpaka sasa makao Makuu hayo yanawatoto 28 ambao wanaume ni 16 na watoto wa kiume ni 12.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo amesena kuwa kuna tatizo kubwa sana la watoto wa mitaani waliokosa malezi bora hivyo anaamini kupitia kuwepo kwa kituo hicho kutaleta matokeo chanya.

"Tuna watoto mil.20 lakini mil. 3 wanaudumavu hivyo tunahaja yakutoa elimu kwa familia"amesema Nyongo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma Antony Mavunde amesema inapofika majira ya jioni katika eneo la Nyerere Square watoto wengi hutandika mabox na kulala chini.

"Ujenzi wa kituo hiki naamini watanufaika maana wengine wanatumia gundi na madawa ya kulevya''amesema Mhe. Mavunde


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com