MAKATIBU WAKUU WA SEKTA YA KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA WA EAC WAKUTANA ARUSHA


Mkutano wa 14 Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Ngazi ya Makatibu Wakuu umefanyika hivi karibuni  jijini Arusha ikiwa ni maandalizi ya mwisho kuelekea Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika jijini hapa tarehe 25 Juni 2021.

Lengo la Mkutano wa 14 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Kilimo  na Usalama wa Chakula pamoja na mambo mengine ni kupitia na kujadili utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Baraza la Mawaziri wa Jumuiya pamoja na kupitia na kujadili masuala mbalimbali  muhimu ya kisera, kimkakati, miradi na program zinazotekelezwa katika sekta ya kilimo.

Katika Mkutano wao, Makatibu Wakuu, pamoja na mambo mengine wamepokea na kupjadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwao na Wataalam ikiwemo, Taarifa ya Usalama wa Chakula ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu Mradi wa Afrika wa Kilimo cha Ushindani cha Mpunga kwa Kanda ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu Maendeleo ya Mifugo; Taarifa kuhusu Mradi wa Kuzuia na Kudhibiti Sumukuvu; Taarifa kuhusu Maendeleo ya Uvuvi; na Taarifa kuhusu Uhamasishaji wa Uchangiaji Rasilimali.

Awali akifungua Mkutano huo, Mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ushirika wa Kenya, Prof. Hamadi Iddi Boga ametoa rai kwa wajumbe wa mkutano huo kuendelea kushirikiana katika kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo kwenye jumuiya  ili kujihakikishia usalama wa chakula.   

Amesema kuwa changamoto nyingi za kilimo zinazozikabili nchi wanachama  zinafanana hivyo ni vizuri nchi zote zikajikita kufanyia kazi changamoto hizo pamoja na kutekeleza program na maazimio yanayofikiwa kwenye mikutano mbalimbali ili hatimaye kuboresha sekta ya kilimo na usalama wa chakula ambayo ni muhimu kwa ustawi wa wananchi.

“Nawashukuru sana kwa kuja na kushiriki kwenye mkutano huu muhimu. Naelewa kwamba usalama wa chakula ni jukumu letu sote kama nchi wanachama na kwa vile tunapitia changamoto zinazofanana ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na corona ni vizuri tukaja na mbinu za pamoja kuzikabili changamoto hizo na kuendeleza sekta hii muhimu ya kilimo” alisema Prof. Boga.

Katika hotuba yake ililiyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Sekta za Uzalishaji katika Sekretarieti, Bw. Jean Havugimana,  Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughilikia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo amewashauri wafanyabiashara wa mazao ya kilimo katika Nchi Wanachama kushirikiana na mamlaka zinazosimamia usalama wa chakula na viwango ili kupata ushauri wa kitaalam kwa ajili ya kuzalisha bidhaa salama na zenye ushindani katika soko. Kadhalika ameshauri elimu kuhusu kilimo itiliwe mkazo kwa nchi wanachama ili kuzalisha wataalam wengi kwenye sekta hii na pia kukuza ajira kwa vijana ambao ni kundi kubwa zaidi katika nchi wanachama.

Kwa upande wake, mwenyeji wa Mkutano huo ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo wa Tanzania, Dkt. Andrew Massawe amewakaribisha na kuwashukuru wajumbe waliosafiri kutoka kwenye nchi zao hadi jijini Arusha licha ya changamoto ya ugonjwa wa Corona  na kuwatakia mkutano mwema na wenye manufaa kwa wananchi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Ngazi ya Makatibu Wakuu umeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Andrew Massawe na kuhudhuriwa pia na Katibu Mkuu  wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatama pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Sekta mbalimbali zinazojishughulisha na masuala ya kilimo na usalama wa chakula hapa nchini.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post