Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MRADI BANDARI YA BAGAMOYO KUFUFULIWA


Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeamua kufufua mazungumzo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na mradi wa Mchuchuma na Liganga ili kuchochea kasi ya kukuza uchumi nchini.

Alisema hayo jana Dar es Salaam alipofungua Mkutano wa 12 wa Sekretarieti ya Baraza la Taifa la Biashara (TBNC)  uliohudhuriwa na wajumbe 50  ambao 25 sekta binafsi na  wengine sekta ya umma. Ulishirikisha pia wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka mikoani, mashirika ya kimataifa na wawekezaji.

Alisema ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ni muhimu kwa sababu utaongeza uwezo wa kushindana na bandari shindani na kukuza uchumi wa Taifa.

Kuhusu mikakati ya kuzisaidia sekta za utalii na usafiri wa anga ambazo zimeathiriwa na ugonjwa wa corona, Rais Samia amesema Serikali imepunguza ada mbalimbali ikiwa ni pamoja na ada ya Wakala wa Wasafirisha Watalii kutoka Dola za Marekani 2,000 hadi Dola 500 kwa kampuni yenye magari kati ya 1 na 3.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sekta binafisi nchini (TPSF), Angelina Ngalula ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujenga mazingira bora na rafiki kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa ikiwa ni pamoja na kufuta baadhi ya kodi na tozo ambazo zimesaidia kuimarisha biashara na uwekezaji nchini.

Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) limeanzishwa likiwa ni jukwaa rasmi la majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kuwezesha kupatikana kwa muafaka wa pamoja kuhusu masuala muhimu yanayohusu maboresho ya Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu za biashara na uwekezaji nchini.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com