Rais Samia Suluhu anatarajiwa kuanza ziara ya kiserikali ya siku tatu mkoani Mwanza, ambapo pamoja na mambo mengine atazindua na kuweka jiwe la msingi kwenye miradi ya maendeleo ya mabilioni iliyoko mkoani Mwanza.
Akizungumza jana juu ya ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Albert Chalamila alisema ziara hiyo itaanza rasmi Juni 13 hadi Juni 15 mwaka huu, ambapo Rais atawasili jijini hapo akitokea mjini Dodoma ambapo atapata fursa ya kufungua mtambo mkubwa wa kusafisha dhahabu
Alisema mtambo huo umejengwa katika Kiwanda cha Mwanza Precious Metal Refinery katika manispaa ya Ilemela kwa gharama ya kiasi Sh bilioni 10.4.
Sambamba na kiwanda hicho pia siku hiyo Rais atafungua jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Kanda ya Mwanza ambao ujenzi wake tayari umekamilika.
"Rais mara baada ya kuzindua jengo hilo la BOT, atapata fursa ya kuhutubia wananchi," alisema Chalamila na kuwataka wakazi wa jiji la Mwanza kujitokeza kwa wingi siku hiyo akisisitiza kuwa hii ndiyo ziara ya kwanza ya Rais mkoani Mwanza baada ya kuapishwa kuwa Rais wa awamu ya sita kwa mujibu wa Katiba baada ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tano John Magufuli kufariki dunia.
Chalamila aliongeza kuwa Juni 14 Rais atakwenda wilayani Misungwi ambapo atazindua mradi wa maji Misungwi uliogharimu kiasi cha Sh bilioni 13.7 na kuhutubia wananchi.
"Baadaye Mheshimiwa Rais atakwenda kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa(SGR) eneo la Fela wilayani Misungwi huo ukiwa ni ujenzi wa loti ya tano," alisema Chalamila na kumshukuru Rais Samia kutokana na kasi na dhamira aliyoionyesha kwenye mradi huo ambapo tayari serikali imeishatoa kiasi cha Sh bilioni 372 ikiwa ni malipo ya awali kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.
Chalamila amefafanua kuwa Juni 15 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan atatembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa daraja la JPM unaojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 699 ili aweze kujionea maendeleo ya ujenzi wake.