Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC BALOZI DKT BATILDA ATOA WIKI MBILI KWA MANISPAA YA TABORA KUSAFISHA NA KUKARABATI MACHINJIO YA KARIKOO


 NA TIGANYA VINCENT
MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani ametoa wiki mbili kwa uongozi wa Manispaa ya Tabora kukarabati na kusafisha Machinjio ya ng’ombe ya Karikoo ili kuweka mazingira mazuri ya utoaji wa huduma.

Alisema hali ya usafi katika eneo hilo hauridhishi na kuongeza ndani ya kipindi hicho uchafu wote yakiwemo maji yanatokana na usafishaji nyama ndani ya Machinjio yaelekezwe sehemu stahili.

Balozi Dkt. Batilda alitoa kauli hiyo leo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kukagua machijio ya Karikoo ambayo ndio yanatoa huduma ya uchinjaji wa ng’ombe , mbuzi na kondoo kwa ajili ya mboga za wakazi wa Manispaa ya Tabora na maeneo ya jirani.

Alisema Manispaa ya Tabora wahakikishe wanaweka malumalu (tiles) kwenye sakafu na kupiga rangi wakati wakisubiri kujenga mradi mkubwa wa kimkati wa machijio ya kisasa.

Balozi Dkt. Batilda alisema sanjari na hilo ni vema wakaboresha ukaushaji wa ngozi ili kuziongezea thamani kuliko ilivyo hivi sasa ambapo zinawekwa kwenye udongo wakati wa ukaushaji.

Aidha alisema uboreshaji wa machinjio hayo utasaidia kutoa huduma nzuri kwa wateja na mapato ya Halmashauri yataongeza kutokana na tozo wanatoza.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tabora Dkt. Yahya Ismail Nawanda alisema watajitahidi kutumia fedha za ndani kukarabati maeneo yote yaliyochakaa na kufanya usafi.

Alisema ndani ya wiki mbili watakamilisha taarifa kwa Mkuu wa Mkoa kuhusu maendeleo ya zoezi hilo.

Awali Mkurugenzi Mtendaji Bosco Ndunguru alisema machinjio hiyo inaweza wa kuchinja ngo’ombe 80 kwa siku.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com