Na Samirah Yusuph
Maswa. Mkuu wa mkoa wa Simiyu,David Kafulila ameagiza kusimamishwa kazi kwa Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Senani iliyoko wilayani Maswa,Ally Kitambulilo kwa kusababisha kifo cha Mama Mjamzito na mtoto.
Agizo hilo amelitoa leo katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG)kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo.
Akizungumza na madiwani wa halmashauri hiyo amesema kuwa amesikitishwa na vifo hivyo vilivyohusisha mama mjamzito na mtoto wakati wa kujifungua kulikosababishwa na uzembe wa Mganga huyo tukio lililotokea Juni 21 mwaka huu saa 2.00 asubuhi.
Amesema kuwa kitendo kilichofanywa na Mganga huyo cha kushindwa kumhudumia Mama mjamzito,Christina Jilala aliyefika kwenye zahanati hiyo kupata huduma na kusababisha vifo hivyo hakiwezi kuvumiliwa hata kidogo.
"Mama huyu amekufa kifo ambacho si mpango wa Mungu pamoja na mtoto kilichosababishwa na uzembe wa Mganga wa zahanati hiyo ambaye hakutekeleza wajibu wake kwa mama huyo aliyefika kwa ajili ya kupata huduma ya kujifungua,"
"Hivyo Nakuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa kumsimamisha kazi Mganga huyo ambaye amesababisha kifo hicho cha Mama na mtoto kwa uzembe na uchunguzi ufanyike juu ya tukio hilo,"amesema.
Amesema kuwa iwapo uchunguzi utabainisha kuwa kuna uzembe umefanyika na kusababisha kifo cha Mama na Mtoto hatua zichukuliwe za kufukuzwa kazi.
Aidha amemtaka Mkuu wa wilaya hiyo,Aswege Kaminyoge kuhakikisha anaisimamia timu ya Afya ya wilaya (CHMT)katika majukumu yao ya kila siku kwani amebaini kuna uzembe mkubwa unafanyika.
Awali Mganga Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dr Mpollo Adorat amesema kuwa Mama huyo alifika katika zahanati hiyo Juni 20 mwaka huu saa 5.00 usiku na kupokelewa na Mhudumu wa Afya wa Jamii.
Mganga huyo alipewa taarifa kwa njia ya simu lakini alimwagiza mhudumu huyo kuwa aendelee kumhudumia jambo ambalo si sahihi.
"Mganga alipopewa taarifa ya kuwepo kwa Mama huyo aliyehitaji huduma ya kujifungua alimweleza Mhudumu wa Afya aendelee kumpatia huduma jambo ambalo si sahihi maana hayo si majukumu yake,"
Dr Adorat alizidi kueleza kuwa Mganga huyo alionekana katika kituo chake cha kazi siku iliyofuatia na kumkuta mama huyo akiwa amejifungua mtoto akiwa amefariki na yeye kufariki muda mfupi baada ya kujifungua baada ya kuvuja damu nyingi kwa kuchanika Shingo ya Uzazi.
Amesema pia baada ya kupata taarifa ya tukio hilo aliondoka na timu ya afya ya wilaya kwenda kwenye zahanati hiyo na kubaini pia kuwa Mganga huyo hakuwepo kwenye kituo chake cha kazi na alitoa taarifa ya uongo juu ya taarifa ya tukio hilo.
Amesema kuwa vifo hivyo vingeepukika iwapo Mganga huyo angekuwepo kwenye kituo chake cha kazi.
Social Plugin