NAIBU Waziri wa Habari,Sanaa na Michezo Mh Pauline Gekul akitoa hotuba ya kufunga Mashindano ya Umitashumta 2021 |
KIKUNDI cha Sanaa cha Mkoa wa Tanga kikitumbuiza kwenye Sherehe za ufungaji wa Mashindano ya Umitashumta leo mjini Mtwara ,Kikundi hicho kimeibuka na ushindi wa kwanza kwenye sanaa ya Ngoma
Na John Mapepele, Mtwara
Naibu waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul (Mb) ameitaka Kamati ya Kitaifa ya UMITASHUMTA na MISSETA kutoa muongozo wa kuhahikisha watoto wa Shule za Serikali na watu binafsi wanashiriki kikamilifu katika mashindano haya ili kujenga umoja, uzalendo na mshikamano kwa watoto wa Tanzania.
Mhe. Gekul ametoa kauli hiyo leo Juni 18, 2021 wakati akifunga mashindano ya UMITASHUMTA kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara ambapo amesisitiza kuwa Malengo ya mashindano haya ni kutoa fursa kwa wanafunzi wa Shule za Msingi kushiriki na kuonesha vipaji vyao vya michezo na sanaa walivyojaliwa na Mwenyezi Mungu.
Amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya michezo hii, mashindano ya 25 ya mwaka 2021 yameratibiwa kwa pamoja na Wizara tatu ambazo ni; Ofisi ya Rais TAMISEMI; Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ambapo amesisitiza kwamba uratibu huu umesaidia kufanikisha maandalizi na uendeshaji wa michezo hii kwa ufanisi mkubwa.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati alipokuwa akifungua mashindano hayo Juni 8, mwaka huu kuhusu kuimarisha ufundishaji wa somo la michezo na michezo katika ngazi zote za elimu Mhe. Gekul amesema.
“Katika kutekeleza hili tunakusudia kufanya yafuatayo; kufanya tathimini ya mitaala ili kubaini mapungufu na kuiboresha, kuhuisha vyuo vya ualimu vya michezo na kuboresha ufundishaji wa elimu kwa michezo kwa vyuo vyote vinavyotoa mafunzo ya ualimu ili wahitimu wake wote wawe na stadi ya ufundishaji wa somo la elimu kwa michezo”.
Ameongeza kuwa tayari, Wizara hizi tatu zipo katika maandalizi ya awali ya kuanzisha tahasusi za elimu kwa michezo kwa kidato cha 5 na 6.
“Hata hivyo imebainika kuwa katika mashindano haya baadhi ya mikoa imewaleta wachezaji ambao hawana sifa ya kushiriki mashindano ya UMITASHUMTA (Mamluki). Jambo hili nalikemea kwa nguvu zote na naelekeza mamlaka za kinidhamu kwa wote waliohusika na jambo hili kuchukua hatua stahiki mara moja. Ili kuhakikisha kwamba suala kama hili halijitokezi tena katika mashindano haya naielekeza Kamati ya mashindano kuhakikisha kuwa muungozo wa uendeshaji mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA unaoandaliwa unaweka utaratibu na kanuni zitakazodhibiti kabisa suala hili” amefoka Mhe. Gekul
Katika mashindano hayo alitoa zawadi mbalimbali kwa washindi wa jumla ambapo mkoa wa Mara uliibuka mshindi wa jumla wakati Mkoa wa Dar es Salaam uliibuka bingwa kwenye fainali za mchezo wa soka kwa wavulana uliochezwa na timu ya Mkoa wa Mara kwa kuichapa Mara magoli manne kwa sifuri mbele ya mgeni rasmi Mhe. Gekul
Mratibu wa mashindano hayo Leonard Thadeo amesema mashindano yam waka huu yamekuwa na hamasa kubwa na kwamba kila mkoa umejitahidi kuonesha kiwango cha hali ya juu tofauti na miaka iliyopita.
Amesema tayari kamatiimeshawachagua wanaliadha kumi waliofanya vizuri ili waweze kushisiki kwenye mashindano ya Dunia ya Riadha kwa wanafunzi kati ya miaka 13-15 yatakayofanyika nchini Serbia mapema Septemba mwaka huu.
Amezizitiza kuwa lengo kubwa la mchezo hii siyo kuangalia ushindi wa kupata kombe bali kuangalia jinsi ya kuwafanya watoto wapate furaha na kujenga misingi ya upendo na uzalendo kwa kizazi cha sasa.
Social Plugin