Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA KUNUFAIKA SOKO ENEO HURU LA BIASHARA AFRIKA


Na Mwandishi wetu, Dar
Serikali ya Tanzania inategemea kunufaika na soko la bidhaa zake katika masoko ya nje baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa ushiriki katika Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA).

Akiongea na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCTA) Mhe. Wamkele Mene, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema kwa sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho kusaini Mkataba wa AfCTA.

“Lengo la ziara ya Mhe. Mene hapa nchini pamoja na mambo mengine ni kukutana na viongozi na wadau wengine muhimu kujadiliana na masuala mbalimbali yanayohusu Mkataba wa AfCTA ikiwa ni pamoja na umuhimu wa Tanzania kuridhia Mkataba huo,” Amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, uanzishwaji wa AfCTA ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa ambapo pamoja na mambo mengine, utekelezaji wake unatarajiwa kuongeza wigo wa fursa nafuu za biashara nchini kwa kuwavutia wawekezaji na kuongeza mauzo hasa ya bidhaa za kilimo.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Sekretariati ya Eneuo Huru la Biashara Afrika (AfCTA) Mhe. Wamkele Mene ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano ambao imempatia tangu wakati wa uchaguzi hadi sasa na kuahidi kuwa utekelezaji wa Mkataba huo utanufaisha kila Nchi Mwanachama.

“……….Naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwani tangu ilipoingia Madarakani imetumia muda mfupi katika kushiriki kwa ukamilifu katika majadiliano ya kusaini mkataba huu na Tanzania imeshiriki vizuri sana kwenye majadiliano haya muhimu,” Amesema Mhe. Wene

Ameongeza kuwa kwa sasa Eneo Huru la Biashara Afrika lina Nchi wanachama 38 ambazo zimekubaliana na Mkataba huo na kwamba kwa sasa Sekretariati hiyo inaendelea kuimarika katika kukuza biashara na sekta binafsi katika nchi wanachama wa AfCTA.

Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika umesainiwa na Nchi 54 kati ya nchi 55 za Umoja wa Afrika ikiwemo Tanzania. mkataba huo ulipata nguvu ya Kisheria Julai, 2019 baada ya nchi 28 kuridhia Mkataba huo. Mkataba wa AfCTA unahusisha maeneno ya ushirikiano katika bishara ya bidhaa, biashara ya huduma, uwekezaji, hakimiliki na ubunifu pamoja na Sera za ushindani.

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameshiriki uzinduzi wa Kongamano la Usawa wa Kijinsia ambapo pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula kongamano hili litakuwa mahsusi kuangalia masuala ya uswa wa jinsia kwa kizazi hiki na kizazi kijacho na kwamba wakuu wa Nchi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa watakuatana Ufaransa katika kongamano hilo kuanzia tarehe 30 Juni hadi 2 Julai 2021.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, Tanzania itashiriki katika kongamano hilo ambapo Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan atawakilishwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango

Uzinduzi wa Kongamano la Usawa wa Kijinsia uliofanyika leo jijini Dar es Salaam umehudhuriwa na Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Fredric Clavie pamoja na Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) Bibi Hodan Addou.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com