Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Tanzia : BINGWA WA MADARAJA YA JUU MHANDISI MFUGALE AFARIKI DUNIA



Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, amefariki dunia leo Juni 29, 2021 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Taarifa zinaeleza kuwa Mhandisi Mfugale aliondoka jana jijini Dar es Salaam na kuelekea Dodoma akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kwa safari ya kikazi ambapo majira ya saa tano asubuhi ya leo, alianza kujisikia vibaya na kukimbizwa hospitali ambapo muda mfupi baadaye, alifariki dunia.

Enzi za uhai wake, Mfugale atakumbukwa kwa kufanya utafiti na kutengeneza mfumo wa madaraja nchini ambapo miongoni mwa madaraja aliyosimamia ujenzi wake ni Daraja la Kikwete lililopo kwenye Mto Malagarasi, Daraja la Mkapa lililopo Rufiji, Daraja la Umoja linalounganisha Tanzania na Msumbiji lililopo Ruvuma na Daraja la Nyerere lililopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Pia Mfugale atakumbukwa kwa kubuni na kusimamia ujenzi wa barabara za kitaifa zenye urefu wa takribani kilometa 36,258 na ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kikosi cha ujenzi wa reli ya kisasa SGR inayoendelea kujengwa.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina!

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com