Na Mwandishi wetu, Dar
Tume ya pamoja ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania na Msumbiji imekutana kujadili masuala ya ulinzi na usalama kati ya Mataifa hayo.
Akiufungua Mkutano huo wa tatu wa Tume ya pamoja ya ulinzi na usalama kati ya Tanzania na Msumbiji Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, amesema mkutano huo ni wa muhimu kwakuwa unatoa fursa ya kuangalia namna ya kukabiliana na matukio yanayotishia ulinzi na usalama yamejitokeza kusini mwa Tanzania na kaskazini mwa Msumbiji ili kwa pamoja kupata suluhisho la kudumu.
“Mkutano wa leo pia utatoa fursa ya kuangalia masuala ya Ulinzi na Usalama, masuala ya mtambuka ambayo ni pamoja na umaskini na utawala bora katika nchi zetu mbili, kikao hiki ni muhimu sana kwani kitarudisha imani kwa wananchi na kuonesha kuwa hatujalala hadi hali itengamae kule Msumbiji,” Amesema Balozi Mulamula
Balozi Mulamula ameongeza kuwa, anaamini kupitia majadiliano yaliyoanza kuanzia tarehe 3 Juni kwa ngazi ya Wataalamu / Makatibu Wakuu hadi leo terehe 5 Juni mkutano wa ngazi ya Mawaziri utapitia mapendekezo ya vikao vya awali kuweza kuchukua maamuzi katika maeneo masuala ya ulinzi, usalama na usalama wa jamiii.
Ujumbe wa Msumbiji umeongozwa na Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji Mhe Jaime Augusto Neto na kuainisha masuala jumuishi kuhusu ulinzi na usalama na kwamba ni Imani yake kuwa kikao hicho kitatoka na maazimio ya utekelezaji ili kuwa na mtangamano imara.
Katika tukio jingine Umoja wa Ulaya umesema unaunga mkono hatua za muendelezo na mabadiliko ya sera za kijamii na maendeleo yanayofanywa Nchini,chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan na kwamba unapongeza hatua hizo.
Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wa Jumuiya ya Ulaya hapa Nchini katika kikao kazi walichokiandaa Jijini Dar es Salaam,Balozi wa Umoja huo Mhe Manfredo Fanti ameongeza kuwa matamko ya Rais Samia kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Jumuiya za Kimataifa,sekta binafsi,uhuru wa kujieleza,haki za binadamu na utawala bora yanatia moyo.
“Matamko na maelekezo ya Mhe. Rais Samia kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Jumuiya za Kimataifa,sekta binafsi,uhuru wa kujieleza,haki za binadamu na utawala bora yanatia moyo na kutuhamasisha kuwashawishi wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza Tanzania,” Amesema Balozi Fanti.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amesema mkutano huo ulikuwa ni wa muhimu kwa kuwa unaweka misingi ya kuaminiana na kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Umoja huo ili kuweka mazingira bora ya Mabalozi hao kuhamasisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka katika Mataifa yao kuja kuwekeza hapa nchini.
Social Plugin