TUME YA UTUMISHI WA UMMA KUWASIKILIZA WATUMISHI NA WADAU KATIKA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA

 

 
Tume ya Utumishi wa Umma inapenda kuwajulisha Watumishi wa Umma na Wananchi wote kuwa katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyopangwa kufanyika kuanzia tarehe 16-23 Juni 2021, kwa nyakati tofauti  itakutana na watumishi wa umma na wadau wake ili kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi  changamoto zinazowakabili kiutendaji.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji amesema umeandaliwa utaratibu ambapo Maafisa wa Tume watapokea na kusikiliza kero na malalamiko ya watumishi wa umma kuhusu masuala mbalimbali ya kiutumishi. Kuanzia tarehe 16 hadi 18 Juni, 2021 Maafisa wa Tume watakuwa Wilayani Kisarawe, Mkoani Pwani na tarehe 21-23 Juni, 2021 watakutana na wadau katika Ofisi ya Tume iliyopo Mtaa wa Luthuli, Jijini Dar es Salaam.

Bwana Muhoji amesema watumishi wa umma na wananchi wanataarifiwa kuwa wanaweza kuwasilisha kero na malalamiko yao kwa kutuma barua pepe kwa anuani ya secretary@psc.go.tz au kupiga simu namba 0738 166 703.

Kupitia maadhimisho haya, Tume inawakumbusha Waajiri, Mamlaka za Ajira, Mamlaka za Nidhamu pamoja na Watumishi wote wa Umma kuhakikisha wakati wote wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na Maelekezo halali yanayotolewa na Serikali.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2021 ni: “Kuheshimu tofauti ya nyenzo za kuimarisha misingi ya utawala wa umma ulio adilifu”

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Tume ya Utumishi wa Umma.

DAR ES SALAAM

14 Juni, 2021

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post