Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo akifanya Mahojiano kwenye kituo cha Redio cha Safari FM mjini Mtwara
Na John Mapepele, Mtwara
Wasanii wa muziki wa kizazi kipya, taarabu na singeli ni miongoni mwa makundi ya wasanii watakaopamba Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISSETA) yanayofunguliwa leo Juni 08, 2021 na Waziri Mkuu, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, amebainisha hayo alipofanya mahojiano na Vituo vya Redio mjini Mtwara leo ambapo amewataja wasanii wa kizazi kipya watakaopamba mashindano hayo kuwa ni pamoja na Ibrah kutoka Konde Gang, Beka Flavour, Peter Msechu na Linah Sanga, pia msanii maarufu wa Singeli Dulla Makabila na Mfalme wa taarabu Mzee Yusuf.
Amesema mashindano ya mwaka huu yanaanza leo na kumalizika Julai 3, mwaka huu, ambapo amesisitiza kuwa lengo la Serikali kwa sasa ni kuendelea kuboresha na kuongeza baadhi ya michezo ambayo itawasaidia kuweza wanafunzi wanapomaliza masomo yao kupata ajira.
“Tunakusudia kuangalia michezo inayoweza kumwandaa kijana kupata ajira baada ya kumaliza shule. Michezo ya maigizo ni miongoni mwa tasnia inakua kwa kasi kubwa hapa nchini ambayo kama mtoto akiandaliwa vizuri anaweza kujiajiri” ameongeza Dkt. Abbasi
Amewataka wazazi kuondokana na fikra potofu ya kwamba michezo haina maana kwa kuwa kwa sasa michezo ni uchumi na ajira kubwa duniani.
Pia Dkt. Abbasi amesema katika mashindano ya sasa wamevialika vilabu, vyama, na mashirisho mbalimbali kuja kuona vipawa na vipaji vya wanamichezo hawa chipukizi
Mashindano hayo yatafanyika katika Viwanja vya Nangwanda Sijaona, Chuo cha Walimu Mtwara (TTC kawaida), Chuo cha Walimu ufundi Mtwara Ufundi Mtwara na katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Mtwara maarufu Mwasandube.
Social Plugin