Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI CHAMURIHO AWATAKA WAKANDARASI WAZAWA KUJISAHIHISHA

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, akifafanua jambo wakati akifungua mkutano wa nne wa mashauriano wa wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2021 ulioandaliwa na Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB), mkoani Mwanza.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, akizungumza na wadau wa Sekta ya Ujenzi walioshiriki mkutano wa nne wa mashauriano ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), mkoani Mwanza.

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhandisi Consolata Ngimbwa, akisisitiza jambo kwa wadau na makandarasi kutoka Sekta ya Ujenzi katika mkutano wa nne wa mashauriano wa Bodi hiyo na wadau hao, mkoani Mwanza.

Baadhi ya wadau wa Sekta ya Ujenzi pamoja na wakandarasi walioshiriki mkutano wa nne wa mashauriano uliondaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho (hayupo pichani) wakati akifungua mkutano huo, mkoani Mwanza.

PICHA NA WUU

.....................................................................................

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, amewataka wakandarasi wazalendo nchini, kuacha ubinafsi na kuungana ili waweze kutekeleza miradi mikubwa inayotolewa na Serikali, kujiongezea uwezo wa ushindani na hatimae kunufaika na fursa zinazojitokeza kwenye soko.

Waziri Chamuriho ameyasema hayo jijini Mwanza wakati akifungua mkutano wa nne na wa mwisho wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi kwa mwaka 2021, ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB).

“Wakati umefika wa kufanya kazi ya ukandarasi kwa lengo la kukua na siyo kupata fedha pekee, suala la kufanya kazi kwa ubia mlipe kipaumbele kwa lengo la kukuza weledi, mitaji na uwezo wa kumiliki mitambo ili mchango wa wakandarasi wa wazawa uzidi kuwa mkubwa kwa kutoa ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa viwanda”, amesisitiza Dkt. Chamuriho.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na kanuni zake kwa miradi yenye thamani isiyozidi Bilioni kumi ili kuhakikisha miradi hiyo inatolewa kwa wakandarasi wa wazawa, aidha Chamuriho amewasihi wakandarasi hao kutoa taarifa za ukiukwaji wa kipengele hiki cha sheria ili sheria ichukue mkondo wake.

Naye Mwenyekiti wa CRB Mhandisi Consolata Ngimbwa, amemshukuru Waziri Chamuriho kwa kushiriki kikamilifu katika vikao vinne vya mashauriano ambavyo vilipangwa na Bodi kwa mwaka 2021 na kufanyika kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Dar es Salaam na sasa jijini Mwanza.

“Mheshimiwa Waziri, Serikali iliamua kutumia force account katika kutekeleza miradi yake na kuacha kutumia wakandarasi baada ya kuona bei za wakandarasi ni kubwa, hivyo bodi imeendesha kozi nyingi za ujazaji wa zabuni kiushindani na sasa wakandarasi hawa wako tayari kushiriki kazi za Serikali”, amesema Mhandisi Ngimbwa.

Kwa upande wake Msajili wa CRB, Rhoben Nkori ameeleza kuwa mkutano huo unalenga kutoa uzoefu wa CRB na wataalamu washauri kuhusu changamoto zinazoathiri ustawi wa wakandarasi, kutoa mtizamo wa wakandarasi na waajiri kuhusu changamoto hizo, kuelezea tathmini ya utekelezaji wa vifungu wezeshi vya sheria ya ununuzi wa umma kwa ukuaji wa wakandarasi pamoja na kujadili fursa za uwekezaji katika dhamana ya Serikali.

Hadi kufikia mwaka 2020 CRB imesajili jumla ya wakandarasi 11,749 pamoja na kusajili miradi 3,179 yenye thamani ya shilingi Trilioni 3.8 ambapo asilimia 46.5 kati ya miradi hiyo ilifanywa na wakandarasi wa ndani na asilimia 53.5 ilifanywa na wakandarasi wa kigeni.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalin, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com