Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda Leo tarehe 4 Juni 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Antony Mtaka akiwa ameambatana na wataalamu wa sekta ya Kilimo ambapo miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya uagizaji wa mafuta ya kula.
Waziri Mkenda amesema kuwa tarehe 13 Juni 2021 Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kuhamasisha kilimo cha alizeti mkoani Singida ikiwa ni njia mojawapo ya kuikabili changamoto ya uagizaji wa mafuta ya kula nje ya nchi.
Waziri Mkenda ameongeza kuwa serikali itaianza safari yake kwa kuboresha huduma za ugani katika mikoa mitatu ya kielelezo ambayo ni Dodoma, Singida na Simiyu kwani Mikoa hiyo ina fursa kubwa ya kuzalisha mazao ya mafuta hususani alizeti na pamba na hivyo itaongeza chachu kubwa ya uzalishaji Alizeti ikiwa ni hatua nzuri kuelekea upatikanaji wa mafuta ya kutosha.
“Tutaanzisha kampeni ya wakulima wakubwa, AMCOS na wakulima wote nchi nzima, Tutawafungamanisha na wanaozalisha mafuta ya alizeti ili wapate mikataba, tutahakikisha wanapata mbegu za kutosha kuhakikisha wanazalisha alizeti” Amekaririwa Prof Mkenda
Katika hatua nyingine Waziri Mkenda amempongeza Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma kwa usimamizi madhubuti katika sekta ya kilimo na kutoa kipaumbele kikubwa katika utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo yam waka 2021/2022.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Antony Mtaka amesema kuwa timu hiyo ya Mkoa wa Dodoma aliyoingoza katika kikao hicho na Waziri wa Kilimo imekusudia kujibu utekelezaji wa hotuba ya Wizara ya Kilimo yam waka 2021/2922 kuhusu kukabiliana na changamoto ya uagizaji wa mafuta ya kula nje ya nchi.
Amesema kuwa mkoa wa Dodoma kupitia Wilaya zinazozunguka Jiji la Dodoma za Kongwa, Chemba na Kondoa ambazo ni wazalishaji wakubwa wa zao la Alizeti wanaingia katika jawabu la kukabiliana na changamoto ya tija ndogo katika uzalishaji wa alizeti pamoja uagizaji wa mafuta ya kula.
“Na sisi kama mkoa tungehitaji tuwe na uwezo wa kuzalisha alizeti kwa tija na kuona namna ambavyo Block Farming inaweza kufanyika kwa ufanisi na namna ambavyo wakulima wetu wadogo wadogo tunaweza kuwafikia ili yale malengo ya wizara yaweze kufanikiwa kwa unafuu zaidi” Amekaririwa Rc Mtaka
Mhe Mtaka amesema kuwa lazima ifike mahala hata kama uagizaji wa mafuta nje ya nchi utaendelea lakini nchi nayo iwe na uhakika wa kuzalisha mafuta kwa wingi ikiwa ni pamoja na kuuza nje ya nchi.