WAZIRI MKENDA AITAKA TFRA KUANDAA MKAKATI WA UPATIKANAJI WA MBOLEA KWA BEI NAFUU


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imetakiwa kuanisha mkakati wa upatikanaji wa mbolea nchini kwa bei nafuu.

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ametoa rai hiyo wakati akizungumza kwenye kikao kazi alipotembelea taasisi hiyo kujionea hali ya utendaji na upatikanaji wa mbolea wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Jijini Dar es salaam.


Pamoja na kuandaa mkakati wa urahisishaji wa upatikanaji wa mbolea, Pia Waziri Mkenda ameitaka taasisi hiyo kuandaa mkakati wa uanzishwaji wa viwanda vipya vya mbolea ili kuongeza uzalishaji wa pembejeo hiyo hapa hapa nchini.

Waziri Mkenda, amesema Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea, ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa uzalishaji wa ndani wa mbolea, unapewa kipaumbele na kwa kuongeza uanzishwaji wa viwanda vipya; mbolea itakuwa ikipatikana kwa urahisi, nafuu na kila Mkulima atamudu kuinunua na kuitumia.

Prof Mkenda ameongeza kuwa Bodi na Menejimenti ya TFRA ibuni mkakati wa namna bora ya kuongeza uwekezaji hapa hapa nchini, kwa kuwa hilo ndiyo suluhisho la kweli katika kuwahakikishia Wakulima wengi wadogo unafuu bei.


Kadhalika, amewataka Watumishi wa TFRA kuongeza udhibiti kwenye usimamizi wa ubora wa mbolea hususan kwenye mikoa yenye matumizi makubwa ya mbolea.
MWISHO





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post