WAZIRI MKUU: HAKUNA MAKINIKIA YANAYOUZWA BILA KULIPIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema makinikia yote yanayosafirishwa yamefuata taratibu na hakuna makinikia yanayouzwa bila kulipiwa kwanza.

“Makontena yote yanayosafirishwa hivi sasa, tayari yameshauzwa na kulipiwa na fedha iko kwenye akaunti zetu. Hapo yako chini ya mnunuzi na yeye yuko huru kuyapeleka anakotaka. Kwa hiyo, Watanzania hatupati hasira. Nataka niwaondolee hofu ya awali… makontena hayo yameshauzwa tayari na hakuna kontena linatoka bila kulipiwa,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa ufafanuzi huo leo (Alhamisi, Juni 3, 2020) Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Msalala, Mheshimiwa Iddi Kassim Idd kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Mbunge huyo alitaka kujua Serikali inatoa kauli gani juu ya makontena yaliyoshuhudiwa yakisafirishwa kupitia barabara ya Bulyanhulu-Kahama na bandari ya Dar licha ya kuwa ilishazuia makinikia kusafirishwa nje ya nchi.

Waziri Mkuu alikiri kwamba Serikali ilishazuia usafirishaji wa makinikia kwenda nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 2017-2018 na kwamba zaidi ya makontena 300 yalizuiwa bandarini kwa sababu wahusika hawakufuata utaratibu na kulikuwa na udanganyifu.

“Makontena hayo yalizuiwa hadi tulipoweka utaratibu mpya, na utaratibu uliowekwa na Serikali ulikuwa kwanza ni kuwatambua nani asafirishe makinikia kwenda nje na nani ametoa vibali hivyo vya kwenda nje.”

“Mheshimiwa Rais wa Serikali ya awamu ya tano aliunda timu ya kufanya uhakiki wa sekta yote ya madini yakiwemo hili la usafirishaji mchanga na makinikia na ikabanikia kwamba ufumbuzi wa suala hilo ni kuunda kampuni ya Kitanzania ambayo ingeshirikiana na makampuni ya nje yaliyopo hapa nchini. Na leo tunayo kampiuni ya Twiga Minerals ambayo imeingia ubia na makampuni ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara yaliyo chini ya Barrick.”

Amesema kuundwa kwa kampuni hiyo kumesaidia Serikali ibaini kuwa kuna aina tano za madini kwenye mchanga unaouzwa. “Baada ya kuchimba, tunapitia kujua aina zote za madini zilizomo. Mwanzo tuliambiwa kuna aina moja tu (dhahabu) lakini sasa tunauza aina zote tano. Tukishapata ule mchanga na kubaini aina zote za madini, kupitia kampuni yetu ya Serikali tunauuza hapa hapa nchini na siyo nje ya nchi.”

Amesema hata bandarini kuna timu ya wataalamu wa kuhakiki nyaraka zote za mauzo tangu yalipofanyika hukohuko kwenye mgodi.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post