WIZARA YA ARDHI,TAA,TCAA NA MIPANGO MIJI DODOMA KUONDOA KERO ZA ARDHI


Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Mendeleo ya Makazi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA), na Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, imekubaliana kuja na mwarubaini wa kuondoa kero za matumizi ya ardhi kwa wakazi na wawekezaji wanaojenga maeneo karibu na viwanja vya ndege nchini.

Kauli hizo zimezungumzwa hivi karibuni na wadau mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma walioshiriki kwenye warsha ya siku moja ya mipango endelevu ya matumizi bora ya ardhi yanayoenda sambamba na uendeshaji wa viwanja vya ndege nchini, iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma.

Mkuu wa Kitengo cha Mazingira cha TAA, Maxmilian Mahangila amesema warsha hiyo inalengo la kuweka sheria sawa kati ya sheria za ardhi, mipango miji pamoja na sheria za masuala ya usalama wa anga, ambapo zimekuwa zikitofautiana kutoka kwenye taasisi moja na kwenda nyingine.

“Ukiangalia hizi sheria zimekuwa zikisigana bila kujua, ambapo ukiangalia sheria zilizowekwa za masuala ya anga zinakataza ujenzi wa majengo marefu, minara na makazi karibu na viwanja vya ndege, lakini sheria za ardhi na hata mipango jiji zinaruhusu ujenzi wa aina yeyote katika maeneo hayo, ambapo hutoa kibali kwa wazawa au wawekezaji kujenga bila tatizo,” amesema.

Hatahivyo, amesema wadau mbalimbali wametoa ushauri juu ya matumizi ya sheria hizo ili ziwe na mtazamo mmoja, ukizingatia sheria na kanuni za masuala ya anga ili kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa kwa kutokuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi.   

Warsha hiyo ilikuwa na mada tatu, ambazo ni “Mipango ya Matumizi ya ardhi yanayoenda sambamba na uchafuzi wa mazingira” iliyowasilishwa na Joyce Kasebele, Afisa Mazingira wa TAA, ambapo amezungumzia mazao yanayoweza kulimwa maeneo yanayozunguka viwanja vya ndege, ambayo hayavutii ndege hai.

Pia amezungumzia  jinsi wananchi wanaoishi maeneo ya kuzunguka viwanja hivyo kuhakikisha wanayaweka katika hali ya usafi, ili kuepusha wanyama na ndege hai kuingia na kufanya madhara kwenye ndege za abiria na mali nyingine.

Naye Meneja wa TCAA wa mkoa wa Dodoma, Ludovic Ndumbaro aliyewasilisha mada ya “Sheria na kanuni za masuala ya anga kuhusiana na matumizi ya ardhi yanayozunguka viwanja vya ndege nchini”.

“Majengo marefu ni hatarishi karibu na viwanja vya ndege, na kila anayejenga maeneo hayo lazima apate kibali maalum kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, baada ya kujiridhisha kama halina madhara ataruhusiwa lakini yale yenye madhara hayawezi kuruhusiwa kwani yanaweza kuzuia ndege wakati wa kupaa na kutua,” amesema Ndumbaro.

Halikadhalika Afisa Mipango Miji Mwandamizi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Edward Mpanda aliyewasilisha mada ya “Mpango wa matumizi ya Ardhi” amesema ndani ya wizara na katika ngazi za wilaya mipango ya matumizi ya ardhi yamezingatia maeneo ya viwanja vya ndege.

“Pamoja na kwamba hizi sheria na mipango ipo wazi kuanzia ngazi ya wilaya na wizarani, lakini imeshughudiwa baadhi ya viwanja vya ndege vimekuwa sio salama kutokana na matumizi mabaya ya ardhi kutoka kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo kuhakikisha majengo yao yanakuwa na urefu wa kawaida ili kuondoa vizuizi vya wakati wa kutua na kuruka kwa ndege,” amesema Mpanda.

Naye Mpima Ardhi Jiji la Dodoma, Hudson Magomba amesema kwa upande wa mpango jiji kumekuwa na mpango wa muda mrefu kuhusuana na  viwanja vya ndege wa mwaka 2010 na baadae kufanyiwa maboresho mwaka 2019-2039.

Hatahivyo, amewataka wananchi kufuata taratibu za ujenzi na kujenga maeneo yaliyopimwa na serikali, na wasivamie maeneo ya viwanja vya ndege kwani ni hatarishi kwa maisha yao.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post