AJALI YA MAGARI MATATU YAUA WATU WATANO, KUJERUHI 6 KIAMBU



Watu watano wanahofiwa kufariki dunia na wengine sita kujeruhiwa vibaya kwenye ajali ya barabarani eneo la Nyambari, Lari kaunti ya Kiambu nchini Kenya leo asubuhi Ijumaa Julai 9,2021

Majeruhi walikimbizwa katika hospitali ya Kijabe ambapo wanapokea matibabu na wamedaiwa kuwa katika hali mahututi. 

Ajali hiyo ilihusisha lori na matatu mbili zenye uwezo wa kubeba abiria 14 kila moja.

 Akithibitisha kisa hicho, kamanda mkuu wa polisi Stephen Kirui alisema idara ya trafiki imeanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo.

 Kirui pia amewataka madereva kuwa waangalifu ikizingatiwa hali ya anga katika sehemu zingine za nchi mwezi huu wa Julai ni mbovu sana. 

"Nimewasiliana na usimamizi wa hospitali ya Kijabe na imethibitishwa kwamba watu 5 walipoteza maisha yao na sita kujeruhiwa vibaya kwenye ajali hiyo," Kirui alisema.

 "Ningependa madereva wote wawe makini na waangalifu, hali ya anga sio nzuri maeneo haya, hatutaki kuripoti maafa zaidi kutokana na ajali," Aliongezea Kirui.

 Kati ya walipoteza maisha yao, watatu ni wanaume ilhali wawili ni wanawake.

 Kwenye taarifa zingine, mama mmoja mwenye umri wa makamo alipoteza maisha yake kaunti ya Homa Bay baada ya kugongwa na lori akiwa amembeba mtoto mgongoni.

 Walioshuhudia ajali hiyo walisema Sharon Otieno alifariki dunia papo hapo kutokana na majeraha ya kichwa huku mtoto wake akikimbizwa katika hospitali ya Ndhiwa akiwa na majeraha madogo.

Chanzo - Tuko News

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
أحدث أقدم