Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Tanzia: ALIYEKUWA MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO ANNA MGHWIRA AFARIKI DUNIA


Aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Elisha Mghwira
Aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, na mgombea Urais nchini Tanzania kupitia Chama cha ACT-Wazalendo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Anna Elisha Mghwira, amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mount Meru, Arusha.

Imeelezwa kuwa Mama Mghwira amefariki dunia leo Julai 22, 2021, majira ya mchana, ambapo taarifa zinadai kwamba wiki moja iliyopita alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Nkoaranga kwa tatizo la kupumua ambapo baadaye hali yake kuwa mbaya alihamishiwa hospitali ya Mount Meru
****

WASIFU WA MAMA ANNA MGHWIRA

Anna Mghwira alizaliwa Januari 23,1959 na amefariki dunia akiwa na miaka 62

Bibi Mghwira alipata elimu ya Msingi katika shule ya Msingi ya Nyerere Road kati ya mwaka 1968 na 1974.

Aidha, alipata elimu ya sekondari katika shule za sekondari za Ufundi ya Ihanja baina ya mwaka 1975 hadi 1978, na shule ya Seminari ya Lutheran baina ya mwaka 1979 hadi 1981.

Huo ulikuwa ndio mwanzo wa safari yake ndefu ya kutafuta elimu. Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, Mghwira alijiunga na Chuo Kikuu cha Tumaini na kuhitimu na shahada ya Theolojia mnamo mwaka 1986.

Bila ya kupoteza muda mwaka huohuo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na huko alihitimu na Shahada ya Sheria.

Mwaka 1999 Mghwira alijiunga na Chuo Kikuu cha Essex nchini Uingereza na mwaka 2000 alipokamilisha masomo yake na alitunukiwa Shahada ya Uzamili ya Sheria.

Na mwaka 2012, Mghwira alijaribu kujiingiza katika Mchakato wa kugombea nafasi ya ubunge wa jimbo la Arumeru Mashariki.

Hata hivyo katika kura ya maoni ya ndani ya Chadema, chama hicho kilimnyima fursa hiyo.

Machi ya mwaka huu, Mghwira aliamua kujiunga na chama kipya cha ACT - Wazalendo. Na katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa chama hicho, Mghwira aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kitaifa wa ACT.

Urais ACT - Wazalendo
Chama cha ACT kilisema kuwa Mghwira ana sifa zote za kuwa kiongozi bora wa taifa la Tanzania.

Ni mtu mwenye upeo mkubwa wa kufikiri, na ana uwezo wa kuwa mlinzi wa taifa. Ni mtu mwenye kiwango kikubwa cha elimu, pamoja na upeo wa uandishi. Kwa mujibu wa chama hicho Mghwira ni kiongozi anayeandika mwenyewe hotuba zake, kutokana na uzowefu wake wa kuandika makala mbalimbali kama mchango katika jamii.

Aliyekuwa mgombea urais 2015 kupitia ACT - Wazalendo Mama Anna Mghwira na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, alitangaza rasmi Ijumaa ya Desemba 8, 2017 kujiunga na chama cha Mapinduzi CCM. Uamuzi huo aliufanya mbele ya hayati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mkutano wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa CCM (UWT).

Katika mkutano huo Anna Mghwira alisema aliamua kufanya hivyo baada ya kuona jitihada za CCM katika kuleta maendeleo, hivyo akaona ni vyema akajiunga nao.

"Mimi baada ya kuwa Mkuu wa Mkoa kwa muda mfupi nimeona mengi ndani ya CCM na nimeona sio mbaya nikitamka kuwa naungana nanyi rasmi, wa muda mfupi nimeiona CCM inayobadilika, nimeona juhudi za kila mtu, ninaiona CCM inayoanza kukataa rushwa, nimeiona CCM inayoanza kulipeleka taifa letu mbeleahsanteni sana kwa kunipokea na kama niliposikia hotuba ya Mwenyekiti ni kweli kuwa sisi akina mama ndiyo wenye jukumu la kubeba nchi. Na mimi naungana na akina mama wenzangu wa UWT wenye malengo ya kuendeleza taifa",alisema mama Anna Mghwira.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com