Benki ya Azania kwa kushirikiana na mfuko wa bima ya afya (NHIF) pamoja na chama kikuu cha ushirika wa wakulima wa tumbaku wilaya ya Chunya, (CHUTCU) wamesaini makubaliano ya kuwawezesha wakulima wa zao hilo kujiunga na bima afya ili waweze kupata matibabu bure.
Makubaliano hayo yamefanyika Julai 19, 2021 kati ya Benki ya Azania Limited,NHIF na CHUTCU katika kata ya Lupatingatinga, halmashauri ya wilaya ya Chunya mkoani Mbeya na kushuhudiwa na mkuu wa wilaya hiyo Mayeka Simon Mayeka.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mwandamizi wa Biashara wa Azania Bank Limited, Jackson Lohay alisema katika makubaliano hayo benki hiyo itatoa mkopo usiokuwa na riba kwa ajili ya kuwawezesha wakulima zaidi ya 700 kupata bima ya afya.
“Katika mkataba wetu tutawawezesha wanachama ambao wapo chini ya
chama kikuu cha ushirika ambao ni zaidi ya 700 lakini watakaonufaika na mpango
ni zaidi ya watu 2000 wanaotegemewa na wanachama,’’ alisema.
Alisema fedha hizo zitarejeshwa baada ya wakulima kuvuna mazao yao
na uyauza.
Mpango w bima kwa wakulima baada ya kuona fedha nyingi za wakulima
zinaishia kwenye kilimo hivyo kushindwa kuwekeza kwenye afya zao hali
inayopelekea kuuza rasilimali zao ili wapate gharama za matibabu wanapopatwa na
maradhi.
“Ugonjwa haupigi hodi ndugu zangu”, alisisitiza.
Hatua hii pia ni ukombozi kwa wakulima wengi, ambao huilisha nchi,
kuingia kwenye mfumo wa bima baada ya kuwa nje ya mfumo kwa muda mrefu.
Makampuni mengi ya huduma za bima yamekuwa yakikwepa kuwapa bima
wakulima kwa madai kuwa biashara zao hazitabiliki (high risk).
Meneja wa NHIF, Mkoa wa Mbeya, Mbala Shitindi alisema mpango huo
utaondoa changamoto za wakulima
kushindwa kupata huduma za matibabu kutokana na kuwa na kipato kidogo.
Aliwasihi wakulima kutumia fursa ya kupata mkopo huo ambao hauna
riba kujiunga na mfuko wa bima ya afya kwa kuwa suala la afya ndio mtaji wao wa
kufanya shughuli za uzalishaji kupitia sekta ya kilimo.
‘’Huo sio mkopo ni fedha ambazo mmeazimwa tu kwa kuwa hauna riba,
naamini itasaidia kuondoa changamoto kwa kuwa wakulima wengi tulikuwa
tunashindw kugharamia sh.76,800 za matibabu kwa mwaka,’’ alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chunya,Mayeka Simoni Mayeka aliishukuru Azania Bank Limited kwa kuamua kuwakopesha wakulima fedha za bima ya afya bila riba na kwamba hatua hiyo inaunga mkono maono ya serikali kuhakikisha wananchi wote wanajiunga na bima ya afya.
“Afya ndio msingi wa kila kitu kama hauna uhakika wa afya yako
hakuna haja ya kupangilia mipango ya mbele na niwaambie tunakoelekea mfumo wa
kutibiwa kwa ‘Cash’ (tasilimu) utaondolewa hivyo ni vyema wananchi wote tuanze
kufikiria kujiunga na bima,’’ alisema.
Baadhi ya wakulima ambao watanufaika na mkopo huo walisema bima
hiyo itawawezesha kuwa na uhakika wa kupata matibabu bure wao na familia zao.
“Tumepokea kwa furaha mkopo huo na umekuja kwa wakati mwafaka kwani
utatuwezesha sisi na familia zetu kupata matibabu bure hata kama hatuna fedha
kwa wakati huo,’’ alisema Grace Mpigauzi mkazi wa Lupa Tingatinga.
Hatua hii ni muhimu sana kwa serikali kupitia Mamlaka ya usimamizi
wa shughuli za bima (TIRA) katika kutimiza lengo la kutoa elimu ya Bima kwa
asilimia 80 ya Watanzania kufikia mwaka 2030, kutoka asilimia 36 ya sasa.
Pia kuongeza idadi ya watumiaji wa bima, kutoka asilimia 15 ya sasa
mpaka asilimia 50 mwaka 2030.
Social Plugin