Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa (kulia) akiongea na Rais wa Benki ya Afrika, Othman Benjelloun, katika Hoteli ya Sofitel, Rabat nchini Morocco
alipofanya ziara ya kikazi nchini humo.
****
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa, ameishukuru Bank of Afrika (BOA), kwa juhudi zake inazofanya kusaidia Tanzania katika sekta mbali mbali za maendeleo Mh. Kassim Majaliwa, alitoa pongezi hizo za shukrani Jumatano Julai 14, 2021 alipofanya mazungumzo na Rais wa Bank of Africa, Othman Benjelloun, katika Hoteli ya Sofitel, Rabat nchini Morocco.
Alisema kuwa uwepo wa Benki hii nchini Tanzania umewezesha wananchi kufaidika na huduma mbali mbali zinazotolewa na Benki hiyo, "Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Rais Samia Suluhu Hassan tunaishukuru Bank of Africa kwa juhudi hizi ".
Aliongeza kwa kumshauri Rais Benjelloun, kuendelea kupanua wigo wa huduma za benki hiyo nchini ili kuwafikia Watanzania wengi, hususani katika sekta za Elimu, Kilimo, Mifugo na Madini.
Waziri Mkuu aliahidi kuwa ataandaa utaratibu wa kukutanisha uongozi wa Benki na sekta binafsi nchini Tanzania ili kuona ni jinsi gani wanaweza kufanya kazi pamoja kuwahudumia Watanzania. Kwa upande wake, Rais Benjelloun alisema lengo la benki hiyo ni kuendelea kukuza uwekezaji wake nchini Tanzania.
"Tuko tayari kuwekeza katika maeneo ambayo viongozi wa kitaifa wa Tanzania watatushauri kwa lengo la kutoa mchango wetu katika kujenga uchumi."
Naye Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, alisema kuwa benki hiyo inapaswa kusaidia kukuza uhusiano wa Tanzania na Morocco katika sekta ya kilimo hususani katika mazao kama mpunga, tumbaku, kahawa na mazao mengine.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Leila Muhamed Mussa, alisema kuna maeneo ya pwani ambayo hayajafanyiwa uwekezaji hadi sasa, hivyo ni fursa kwa wawekezaji kuyatumia na kwamba Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi amefungua milango kwa wawekezaji.
Aliitaka benki kuona jinsi ya kuwezesha wakulima utekelezaji shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Pamoja na ushiriki wa benki katika miradi mbalimbali ya maendeleo, benki imeonyesha dhamira yake katika kusaidia Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) kwa kutoa bidhaa na huduma zinazovutia wateja wake. Kama benki ya biashara Imekuwa ikihudumia wateja wa makundi ya wateja wa Rejareja, Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) na wateja wa Makampuni.
Social Plugin