Watu wawili wamefariki dunia baada ya kuingia na jiko la mkaa katika chumba cha kulala kwa ajili ya kupunguza baridi mkoani Njombe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issah amewataja waliofariki dunia kuwa ni Benitho Mbatha (23) mpiga debe wa mjini Njombe na Jazila Said (27) mkazi wa Namtumbo mkoani Ruvuma.
“Baada ya kufariki hakuna mtu ambaye aligundua kama kuna watu wamefariki, tukio hili limetokea Julai 17,2021 majira ya saa tano nusu usiku huko mtaa wa National Housing kata ya Njombe mjini wakiwa wamelala kwenye chumba kimoja,”amesema Kamanda Issah.
Amesema sababu ya kifo chao inaonyesha wakati wakiwa hai waliweka moto wa mkaa kwa ajili ya kujihifadhi na baridi ambapo mtindo huo umekuwa ukitumika na watu wengi mkoani Njombe.
Mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi marehemu Benitho Mbatha, Amani Samsoni amesema yeye alikuwa wa kwanza kushuhudia tukio hilo baada ya kwenda kumtembelea marehemu na kuwaona wote wawili wakiwa wamefariki
“Lakini bado mimi nilifuatilia kwa majirani wanasema yule mwanamke alikuwa anaelekea Madaba,alikosa nauli na huyu kijana kwa kuwa yupo pale kwenye magari akamwambia njoo upumzike kwanza na kesho nitakusaidia nauli ya kukufikisha kwenu kwa hiyo hiki kitu kinahuzunisha sana”,amesema Samson.
Nao majirani akiwemo Winfrida Msalilwa wamesema “Marehemu huwa anapenda sana kuja hapa na alikuja pia akachukua moto na akachukua chipsi mayai akasema nina mgeni wangu huko ndani lakini siku baada ya siku tukashangaa haonekani mpaka tulipoona wanakuja polisi".