Na Jackline Lolah Minja Morogoro.
Waumini wa Dini ya Kikristo nchini wamesisitizwa kutouogopa ugonjwa Corona badala yake wachukue tahadhari ili kuweza kuushinda kwa maslahi ya Watanzania wote.
Akitoa salamu kwenye Ibada maalumu ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Kanisa katika mtaa wa Bethania Usharika wa Mji Mwema Morogoro ,Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Morogoro Jacob Ole Mameyo amesema kwa sasa janga hilo limekuja kwa utofauti kuliko awali hivyo ni vyema kujilinda na kulinda wengine.
"Mwanzo Corona ilinyanyasa wazee , lakini sasa inamaliza hadi watoto hivyo nawasihi kujilinda na tusiiogope , Makuhani tuhakikishe tunalinda waumini wetu kutokana bila wao hatutaweza pata mapato kwa kuendeleza Kanisa." Alisema mameyo
Katika hatua nyingine Askofu Mameyo amesema lazima Wakristo kudumisha upendo ili kutimiza kusudi la Mungu kwa wanadamu na kuepusha migogoro katika kanisa.
"Baadhi ya watu wamebadilisha maneno ya Biblia kuwa mpende jirani yako kama nafsi yako wanasema mpende jirani yako kama unanafasi hii sio sahihi, hivyo sio agizo la Mungu tusifanye ujanja ujanja badala yake tuzidi kumbembeleza Mungu atupokee kwenye uzima wa milele kwa kuwa hili ni agizo kuu kwetu wanadamu", alisema askofu Mameyo.