Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe (UWT) Scolastika Kevela.
***
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe (UWT) Scolastika Kevela amevitaka vyama vya upinzani kuacha kuleta chokochoko nchini kwa kigezo cha kutaka katiba mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Kevela ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, alisema Rais Samia Suluhu Hassan alishatolea ufafanuzi suala hilo kwa kusema kuwa apewe muda hivyo wanapaswa kutulia.
Alisema kauli hiyo ya Samia ilipaswa kuheshimiwa na kupokelewa kwa mtazamo chanya na wananchi wote hususani wale wanaoleta chokochoko hususani wapinzani hao ambao muda mwingi wamekuwa wakianzisha wakitafuta sababu za kuanzisha chokochoko.
"Rais Samia aachwe afanye kazi yake tuliyomtuma wananchi wananchi kwa mujibu wa katiba, ndiyo kwanza uongozi wake una miezi minne madarakani, hizi kelele za wanaotaka katiba zinatolewa kwa lengo la kutaka kumtoa katika reli ya kuwatumikia watanzania", alisema Scolastika.
Aidha alisema anashangazwa na wapiga kelele hao kuanza kujitokeza kwa wingi na kuleta chokochoko hizo ndani kipindi hilo kifupi cha uongozi wa Rais Samia tofauti hali ya kuwa kabla yake kulikuwa na kiongozi mwingine katika nafasi hiyo lakini hawakuthubutu kufanya hivyo.
"Mimi kama Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe nalaani chokochoko hizo na zaidi nawaomba watanzania wote wenye mapenzi mema na nchi hii kuendelea kuunga mkono juhudi anazozifanya Rais wetu kutuletea maendeleo Watanzania wote" ,alisema Scolastika.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huo amempongeza Rais Samia kwa juhudi mbalimbali anazoendelea kuzichukua katika kuhimarisha mahusiano ya kidiplomasia na mataifa mengine duniani
Alisema kitendo cha Rais huyo kukutana na viongozi kutoka mataifa mbalimbali na wakati mwingine kufanya ziara katika mataifa hayo, kunaonyesha dhamira yake ya kushirikiana na mataifa hayo katika masuala mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa uchumi.