Mwanafunzi wa taasisi ya kimatibabu kaunti ya Homa Bay, KMTC nchini Kenya Emily Chepkemoi (23) aliyeripotiwa kutoweka kwa siku mbili amepatikana akiwa amefariki dunia ndani ya nyumba yake ya kupanga.
Kulingana na wanafunzi wenzake, Chepkemoi ambaye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza alitoweka siku ya Ijumaa, Julai 2 baada ya kuwa darasani, mwili wake ulipatikana Jumapili, Julai 4 baada ya kutafutwa na familia.
"Marehemu alikuwa darasani siku ya Ijumaa na akaenda nyumbani kwake majira ya jioni, alibadilisha nguo na kuenda kuteka maji, baada ya hapo sikumsikia tena hadi nilipopokea habari kwamba alikuwa ameaga dunia," Mwanafunzi mwenzake alisema.
Kwa mujibu wa taarifa za Daily Nation, milango ya nyumba yake ilikuwa imefungwa na mwili wake ulipatikana ukiwa umefungwa kwenye blanketi ukiwa na majeraha kadhaa.
Marafiki wake waliambia maafisa wa polisi kwamba, Chepkemoi alikuwa ameweka muziki kwa sauti ya juu na hawangeshuku kwamba alikuwa hatarini.
"Mimi sikusikia chochote, nilidhani kulikuwa na sherehe kwake kwa sababu pia sikusikia kelele zozote za kutisha," Mmoja wa marafiki wake alisema.
Kwa mujibu wa taarifa ya chifu msaidizi wa Homa Bay mjini, Dancan Oketh, Chepkemoi alidunga kisu mara kadhaa kabla ya kufariki dunia.
"Alikuwa na majeraha kadhaa ya kisu kwenye kichwa chake, mgongo na shingo, alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi, Chifu huyo alisema.
Mwili wake ulipelekwa katika makafani ya hospitali ya rufaa ya Homa Bay huku upasuaji wa maiti ukisubiriwa kufanyika.
Chanzo - Tuko News
Social Plugin