Na
Mwandishi Wetu
Waziri
wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile (Mb)
na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo mheshimiwa Innocent Bashungwa
(Mb) wamezindua Mfumo ulioboreshwa wa utoaji Leseni wa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) ambao utawezesha waombaji wa leseni kubwa za mawasiliano
kuwasilisha maombi ya leseni kwa njia ya mtandao.
Waziri
wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amebainisha kuwa sekta ya Mawasiliano
kwa sasa inapitia mabadiliko makubwa na kwamba Serikali imeazimia kufanya
mabadiliko makubwa ya uwekezaji katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
TEHAMA na Mawasiliano, na kwamba mfumo huo ulioboreshwa wa uchakataji leseni za
Mawasiliano utawezesha upatikanaji wa leseni kwa haraka na kuvutia uwekezaji
katika sekta za Mawasiliano,TEHAMA na utangazaji.
“Kwa
hiyo na sisi kama Wizara tunaendelea kujipanga kuhakikisha kwamba tunaboresha
mifumo yetu ili kuhakikisha kwamba sisi kama wizara hatuwi kikwazo kwao”
alisema waziri Ndugulile.
Ndugulile
alibainisha kuwa mfumo huo umeboreshwa na kwamba maombi ya leseni ndogo za
Mawasiliano kwa akali zitachukua siku tano kuanzia maombi hadi kukamilika kwa leseni ikiwa mwombaji
atakuwa amekamilisha taratibu zote za maombi; kwa upande wa leseni kubwa zitatumia siku Arobaini na Tano hadi
kukamilika hatua ambayo Waziri Ndugulile amesema ni ya kupongezwa kwa kazi
kubwa ambayo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imefanya hadi kukamilisha kazi ya
kuboresha mfumo huo uliobuniwa na kuundwa na wataalamu wa TEHAMA wa TCRA.
“Tunaamini
mfumo huu utaongeza uwajibikaji na uwazi kwa sababu kila mmoja atakuwa anaona”
alisisitiza Ndugulile na kuongeza.
Waziri
Ndugulile alibainisha kuwa Wizara yake kwa pamoja wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo zimeazimia kuhamasisha uwekezaji hasa katika sekta ya
Utangazaji hususani katika usikivu wa redio ambapo hivi karibuni wizara ilitoa
tangazo la maombi kutoka kwa wananchi wenye nia ya kuwekeza katika utangazaji
kwenye wilaya Sitini na Tisa za Tanzania bara.
“Niendelee
kutoa rai kwa wawekezaji kwamba sasa hivi tumefungua milango ya uwekezaji
katika sekta ya Mawasiliano na TEHAMA ikiwa ni pamoja na mawasiliano ya simu,
utangazaji na huduma za posta ambazo tunazisimamia kwa hiyo yeyote anaehitaji
kuwekeza tunawakaribisha sana” alisisitiza Ndugulile.
Ndugulile
alitumia fursa hiyo kuahidi kwamba Wizara yake inaenda kufanya mabadiliko
makubwa katika mfumo wa utoaji leseni sanjari na kufanya mabadiliko ya tozo za leseni
zikiwemo leseni za maudhui mtandaoni, huku akibainisha kuwa mabadiliko ya tozo
yatakuwa tayari ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.
Nae
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Innocent Bashungwa alibainisha
kuwa wizara anayoisimamia inayo matumaini kuwa mfumo huo wa leseni utaleta
mabadiliko makubwa ya kiutendaji hasa katika eneo la uwazi na uwajibikaji.
“mfumo
huu unaleta mageuzi makubwa;nimependa ile hali ya uwazi wa mfumo huu wa leseni
hii itatusaidia kwenye uwazi ; lengo la wizara hizi mbili ni kuleta ufanisi na
kuwa na customer care approach (mrengo wa kuwajali wateja)” alibainisha Waziri wa
Habari.
Chini
ya mfumo wa utoaji leseni ulioboreshwa; Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inatoa
leseni za aina kuu mbili ambazo ni Leseni kubwa (Individual licence) na Leseni
ndogo (Class licence); leseni kubwa zimegawanyika katika makundi yafuatayo Leseni
ya vifaa/miundombinu ya mtandao wa Mawasiliano- (Network Facility License -
NFL); Leseni ya huduma za mtandao wa Mawasiliano- (Network Services License -
NSL); Leseni ya matumizi ya huduma za Mawasiliano- (Application Services
License - ASL); Leseni ya maudhui ya Utangazaji (Content Services License -Televisheni na Redio). Leseni ndogo ni
pamoja na Maudhui Mtandaoni (redio na televisheni za mtandaoni, blogu, mitandao
ya kijamii na majukwaa mtandaoni); Televisheni za waya (Cable Television); Kuingiza
vifaa vya mawasiliano; Kusambaza vifaa vya mawasiliano; Kuuza vifaa vya Mawasiliano;
Ufungaji/ujengaji na matengenezo ya vifaa vya mawasiliano; Ungo wa mawasiliano
(VSAT); Mawasiliano ya Redio kwenye Ndege; na Mawasiliano ya Redio kwenye Meli.
Mwombaji wa leseni anaweza kuwasilisha maombi yake ya leseni kupitia mfumo huo
unaopatikana kwenye tovuti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kupitia kikoa cha
www.tcra.go.tz.