WATATU WA FAMILIA MOJA MBARONI TUHUMA ZA KUMUUA MAMA YAO KUWA NI MCHAWI




Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Tuntufye Mwakagamba

Watu watatu  wa familia moja wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera kwa tuhuma za kumuua Mama yao mzazi Frazia Rukera (99), mkazi wa Kijiji cha Mkombozi kata ya Rukuraijo wilayani Kyerwa kwa kumkata kichwa, miguu na mikono  kwa kile kilichodaiwa walikuwa na ugomvi wa muda mrefu uliotokana na kumtuhumu kuwa mchawi.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Tuntufye Mwakagamba, amesema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 07 mwaka huu, majira ya saa 10:00 alfajiri wakati Bibi huyo akiwa amelala ndani peke yake, na kwamba baadhi ya viungo vilivyokatwa kutoka katika mwili wa Bibi huyo ambavyo ni kichwa, mguu mmoja na mkono mmoja havijapatikana.

Amewataja watuhumiwa wanaoshikiliwa kuwa watoto wa bibi aliyeuawa  ambao ni Laurent Francis (60) na Alexander Francis (55) pamoja na shemeji yao Agness Gidioni (70) wote wakazi wa Kijiji cha Nyabirungu wilayani Kyerwa.

Kamanda Mwakagamba amesema kuwa bibi huyo tayari amekwishazikwa bila kuwa na baadhi ya viungo vyake ambavyo vinaendelea kusakwa na polisi.

Hata hivyo, Kamanda Mwakagamba ametaja sababu za kuwashikilia watoto wa marehemu kuwa ni kutokana na kuwepo kwa madai ya kuwepo kwa ugomvi wa muda mrefu na mama yao ambapo,wamekuwa wakimtuhumu kuwa ni mchawi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post