Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI AKERWA NA MRUNDIKANO WA BODABODA VITUO VYA POLISI


Na Abubakari Akida,MOHA

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo amesikitishwa na uwepo wa idadi kubwa ya bodaboda katika Vituo mbalimbali vya Polisi nchini huku akiwaasa wananchi ambao mashauri yao yanasikilizika wafike katika vituo hivyo ili kuondoa msongamano wa vyombo hivyo.

Ameyasema hayo leo Visiwani Zanzibar baada ya kupata maelezo na kutembelea karakana ya kuhifadhia vidhibiti hivyo katika Kituo cha Polisi Madema ambapo amesikitishwa na wingi wa bodaboda kituoni hapo.

“Nchi yetu inataka kupiga hatua za kmaendeleo na uchumi, kwa namna hii ya mrundikano wa bodaboda katika vituo vya polisi maana yake shughuli nyingi huko za vijana zimesimama, naelewa kuna vidhibiti kwa ajili ya kesi maalumu ambazo nyingine ziko mahakamani hivyo haviwezi kuachiwa lakini kwa vile ambavyo kanuni na sheria inaweza kuviruhusu basi viondoke, natoa wito kwa wananchi kufika vituo vyote vya polisi nchi nzima na kufanya mazungumzo na wakuu wa vituo ili tuondoe mrundikano huu,kila mkoa ninaotembelea nakuta vituoni kuna mrundikano wa bodaboda,wananchi njooni muonane na wakuu wa vituo mchukue vyombo vyenu”, alisema Naibu Waziri Chilo.

Akizunguma katika ziara hiyo,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Unguja, Awadh Juma Haji amesema vyombo vingi vilivyopo kituoni ni kutokana na waliovitendea makosa kutofika vituoni kwa wahusika wakuu hali inayopelekea uwepo wake hapo ambapo alikiri imekua ni kero kwa jeshi la polisi.

“Mheshimiwa Naibu Waziri hapa vyombo vilivyopo ambavyo tunavishikilia hatuwezi kuvitoa ni vile ambavyo mashauri yake bado yapo mahakamani lakini kuna vingine watuhumiwa wake wamekimbia tangu vikamatwe bado awajajitokeza tunachofanya tunasubiri ule muda wa kisheria wa miezi sita ili taratibu za utaifishaji zifanyike hapa tuna magari ya wizi,bodaboda nyingine zimeshiriki katika makosa ya usalama barabarani nyingine zimehusika kwenye uporaji na tatizo linguine wahusika hawaji vituoni kuonana na wakuu wa vituo kuchukua vyombo vyao hali hiyo upelekea mrundikano huu”,alisema RPC Awadh.

Akitoa hali ya ulinzi na usalama katika Kipindi hiki cha Sikukuu Kamanda Awadh amesema Sikukuu ya Eid imesheherekewa vizuri pasipo kuwepo matukio makubwa ya uhalifu huku Jeshi la Polisi likiendelea na doria zake za kawaida katika kuhakikisha amani na usalama vinakuwepo katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com