TAKUKURU YAANZA KUCHUNGUZA MABILIONI YA FEDHA MANISPAA YA SHINYANGA


Mkuu wa TAKUKURU mkoani Shinyanga Hussen Mussa akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari.

Na Mwandishi wetu, Shinyanga.
TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Shinyanga, imeanza kuchunguza matumizi ya fedha kiasi cha shilingi bilioni 31.161 zilizotolewa na Benki ya Dunia (WB) kwa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Shinyanga, Hussein Mussa uchunguzi huo unatokana na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyotolewa hivi karibuni.

Mussa amesema, katika ukaguzi maalumu uliofanywa na CAG ilibainika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ilipokea jumla ya sh, bilioni 31,1kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo, kiasi cha sh. bilioni 26,1 ni fedha zilizotolewa na Benki ya Dunia na sh. bilioni 4,9 kutoka vyanzo vingine.

Alisema kutokana na taarifa ya ukaguzi maalumu kwa kipindi cha miaka mitatu imeonekana kuna mapungufu katika matumizi ya fedha hizo kwenye utekelezaji wa baadhi ya miradi hivyo TAKUKURU inachunguza ili kuthibitisha iwapo kuna ubadhirifu uliofanyika kwenye matumizi ya fedha hizo.

“Tumeanza kuchunguza hoja zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika ukaguzi maalumu alioufanya katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, ukaguzi huo unahusisha kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2017/2018 hadi 2019/2020 mwaka wa fedha wa Serikali,” alieleza Mussa.

Aliendelea kueleza katika kipindi cha robo ya nne, Aprili mpaka Juni 2020/2021 Ofisi yake ilifuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayopewa fedha za Serikali pamoja na ufadhili wa wadau wa maendeleo ambapo jumla ya miradi 14 yenye thamani ya sh, bilioni 7,0 ilifuatiliwa.

“Katika miradi hiyo 14 tulibaini mradi mmoja una mapungufu ambapo TAKUKURU tulitoa ushauri kwa mamlaka husika na ushauri ulifanyiwa kazi, miradi tisa imekamilika na ipo vizuri minne inaendelea ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake,”

“Kwa upande wa malalamiko ya rushwa, idara ambazo zimeendelea kulalamikiwa katika kipindi hiki cha robo ya nne, Serikali za mitaa zimeongoza kutokana na malalamiko 22 yaliyopokelewa, Ardhi (4), Polisi (3), Elimu (3), Ujenzi (2), Biashara (2), Maji (2), Mifugo (2), Misitu, Mifugo na Mahakama lalamiko moja moja,” alieleza.

Katika hatua nyingine Mussa amewatupia lawama baadhi ya watu wanaombwa rushwa ya ngono kwa kuogopa kutoa taarifa katika Ofisi yake ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria hii ni pamoja na baadhi ya wazazi ambao watoto wao hupewa mimba.

“Hili la rushwa ya ngono kwetu ni agenda ya kudumu, maana ina athari kubwa kwa nchi yetu na jamii kwa ujumla, inaweza kutuletea madhara kwenye utumishi wa umma, sekta binafsi, vyuoni na hata kutuletea wasomi wasiokidhiti na wataalamu wanaoajiriwa kutokuwa na sifa,”

“Hivyo nitoe wito kwa wananchi, waache tabia ya kutokutoa taarifa, maana wana mazoea ya kuficha mambo na hawataki kutoa ushirikiano hasa baadhi ya wazazi ambao watoto wao hupewa mimba na kufukuzwa shule, lakini hawataki kuwataja watuhumiwa wakihofia kukosa mtu wa kulea mtoto,” alieleza Mussa.

Akifafanua alisema wapo baadhi ya watuhumiwa hujitahidi kutoa fedha kidogo kwa wazazi wa watoto waliobebeshwa mimba lakini fedha hizo huwa ni kidogo na za matumizi ya muda mfupi tu na baada ya hapo watuhumiwa hao hawaendelei tena kumuhudumia mtoto aliyezaliwa wala mama yake ambaye tayari amepoteza haki yake ya kupata elimu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post