Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TGNP YATOA MAFUNZO KWA VITUO VYA TAARIFA NA MAARIFA DAR ES SALAAM, SANGAI ATAKA WATAMBUE RASILIMALI ZA NCHI


Afisa wa Programu ya Mafunzo na Ujenzi wa Nguvu katika Jamii wa TGNP Bi. Anna Sangai akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wanajamii kutoka vituo vya taarifa na maarifa vya mkoa wa Dar es salaam.

***
Wanajamii wametakiwa kuamka na kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka ili kuweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao.

Hayo yameelezwa jana Julai 15,2021 na Afisa wa Programu ya Mafunzo na Ujenzi wa Nguvu katika Jamii wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Bi. Anna Sangai wakati akitoa mafunzo kwa baadhi ya vituo vya Taarifa na Maarifa vya mkoa wa Dar es salaam.

Akiongea katika mafunzo hayo ya siku moja yaliyofadhiliwa na Chuo cha COADY International kupitia mradi wake wa Engage: Woman Empowerment and active Citizen, wenye lengo la kuisaidia jamii kuweza kuzitambua na kuzitumia fursa mbalimbali walizonazo katika maeneo yao kwa kutumia moduli ya ABCD.

Afisa huyo amesema kuwa moduli hiyo licha ya kuwasaidia wanajamii kuweza kutambua fursa mbalimbali ndani ya jamii yao, lakini pia itawasaidia kuweza kupigania usawa wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kuhimiza serikali kuweza kutenga bajeti yenye mlengo wa kijinsia.

Amesisitiza kuwepo na bajeti yenye mrengo wa kijinsia kwa kuwa itakuwa ni bajeti inayolenga makundi yote lakini pia inahakikisha rasilimali fedha zinazokwenda kutumika kwenye miradi ya maendeleo zinatumika kama zilivyokusudiwa.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo ya ABCD yamewakutanisha wanajamii kutoka katika vituo vya Taarifa na Maarifa Kipunguni, Majohe, Saranga Mabwepande, Mabibo na Kivule ambapo vituo hivi vilifanyiwa uraghibishi mwezi Machi mwaka huu, na hii ni kuendelea kuwajengea uwezo ili waweze kuendelea kutekeleza mpango kazi waliyouandaa baada ya mafunzo yaliyopita.

Aidha Sangai amesema kuwa mafunzo hayo pia ni fursa ya wanajamii hao kuweza kubadilishana uzoefu wakati wa utekelezaji mpango kazi huo, kwa kushirikishana na kusaidiana endapo kituo kimoja kitakuwa kimekwama au kinapitia kwenye changamoto ama nyingine.

Amesema kuwa matarajio yao baada ya mafunzo haya ni kwamba watakuwa wameweza kuzalisha waraghibishi wazuri na wengi ambao wataweza kuwa mabalozi wazuri wa kwenda kuwafundisha wenzao ambao hawajaweza kupata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo.

Afisa wa Programu ya Mafunzo na Ujenzi wa Nguvu katika Jamii wa TGNP Bi. Anna Sangai akiwezesha katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wanajamii kutoka vituo vya Taarifa na Maarifa vya Dar es salaam.
Baadhi ya wanajamii wakisikiliza kwa umakini mafunzo ya ABCD.
Mshiriki kutoka kituo cha Taarifa na Maarifa Kipunguni Fatma Abdulahman akichangia mada katika semina ya ABCD iliyoandaliwa na TGNP.
Baadhi ya wanajamii walioshiriki mafunzo ya ABCD yaliyoandaliwa na TGNP wakiwa katika kazi za makundi.
Mwanaharakati kutoka kituo cha taarifa na maarifa Majohe Joseph Safari akitoa ufafanuzi wa jambo katika semina ya ABCD.
Semina ikiendelea

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com