Na Dotto Kwilasa,Dodoma.
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetoa mafunzo ya uelewa wa udhibiti wa masuala ya Nishati na Maji kwa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA) huku ikiwa na matarajio kuwa semina hiyo itawasaidia kutimiza azma ya Serikali katika kuwasaidia watanzania kutambua haki na wajibu wao kwa jamii na kwa Serikali yao.
Mafunzo hayo yametolewa kwa Wanachama 60 ,ambapo 3o kati yao ni wadau wa moja kwa moja kwa Mamlaka hiyo kwa kuwa na taaluma ya mafundi umeme huku wakitegemewa kutoa huduma bora zaidi kwa jamii katika kukidhi mahitaji ya ajira binafsi.
Akizungumza leo Julai 20,2021 jijini Dodoma wakati akifungua semina hiyo iliyoandaliwa na EWURA kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka , Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi amesema anaamini semina hiyo itawasaidia kutimiza azma ya Serikali katika kuwasaidia watanzania kutambua haki na wajibu wao kwa jamii na kwa Serikali yao.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema , mojawapo ya majukumu ya EWURA ni pamoja na kujenga uelewa kwa watumia huduma ili wafahamu haki na wajibu wao.
Pamoja na hayo Dkt. Mkanachi ameitaka EWURA kuendelea kujenga uelewa kwa watumiaji wa huduma mbalimbali ili wafahamu haki na wajibu wao katika kuchochea maendeleo na kukuza uchumi.
“Ninafahamu kuwa ninyi ni sehemu muhimu yawatumia huduma za EWURA,inawezekana kuna mafundi umeme humu ndani ambao inabidi wawe na leseni ya EWURA vilevile inawezekana kuna wamiliki wa vituo vya mafuta ambao inabidi wawe na leseni za EWURA au tunaweza kuwa na wamiliki wa kampuni za kuzalisha na kusambaza umeme na sote tunatumia maji na umeme huduma ambazo zinadhibitiwa na EWURA,”amesema.
Amesema kwa niaba ya Serikali wanatoa shukrani za dhati kwa Menejimenti ya EWURA kwa kukubali ombi la kutoa mafunzo hayo kwani kwa kufanya hivyo wananchi wenye ulemavu wa kusikia watakuwa wanaelewa shughuli za EWURA na mafundi umeme wataweza kutimiza matakwa ya kisheria na kikanuni katika shughuli zao.
Kwa upande wake,Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo kwa Viziwi Tanzania (TAMAVITA) Bw.Kelvin Nyema,amesema kuwa chama chao kimefikia hatua ya kuomba kupatiwa mafunzo hayo ili wajengewe uwezo mafundi umeme na mafundi wa nyumba ambao ni viziwi.
“Miongoni mwa viziwi wapo mafundi wa umeme, mafundi ujenzi wa nyumba na tunajua tunahitaji leseni lakini hatujui nini cha kufanyeje, pia viziwi ni watumiaji wa maji na nishati na ndio maana tunahitaji mafunzo,”amesema.
Awali akiwasilisha mada,Meneja Mawasiliano na Uhusiano EWURA,Titus Kaguo ameeleza kuwa Mafunzo hayo yametolewa kutokana na uongozi wa TAMAVITA kuomba kupewa elimu na uelewa wa masuala ya udhibiti wa nishati na maji hali itakayolenga zaidi kuchochea maendeleo.
Kwa umuhimu huo Kaguo amezishauri Taasisi nyingine kuona umuhimu wa kutoa mafunzo kwa makundi maalumu ili kuleta hamasa kwa jamii kuwasaidiakatikakutekeleza majukumu ya uzalishaji na kujiiunua kiuchumi.
“Nazishauri Taasisi nyingine kutowaacha wenzetu hawa ambao wanaonekana kama ni watu wa pembeni waliosahaulika kwani nao wana uwezo wa kutumika kujenga uchumi wa nchi yetu,”amesisistiza Meneja huyo wa EWURA.
Pamoja na mambo mengine ameongeza kuwa hatua hiyo ya mafunzo imekuja kwa kuzingatia kuwa kundi hilo ia ni wadau muhimu kwa Taasisi hiyo ambapo kati ya Wanachama hao 60 ,3o kati yao ni wadau wa moja kwa moja kwani wana leseni za Ewura hivyo.
“Na kwa kuwa hapa tuna mafundi umeme 30 basi tunategemea huduma bora zaidi kutoka kwenu na kuongezeka kwa ajira binafsi,tumetimiza wajibu wajibu wetu kuwajenga na kuwaelimisha ili wawe mabalozi kwa wenzao,jamii imekuwa na tabia za kuwasahau wenzetu wa makundi maalum kwa kufanya hivi itasaidia makundimaalumu kuheshimika na kushirikishwa katika uchumi wa viwanda,”amesema