JAJI MKUU PROF. JUMA AKIPONGEZA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO KUANDAA KITABU CHA MKUSANYIKO WA MASHAURI YA WATOTO


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaohudumia Watoto (UNICEF), Bi. Sampathi Perera.

Na Rosena Suka IJA Lushoto
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa pongezi kwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kuandaa Kitabu cha Mkusanyiko wa Mashauri ya Watoto (Compendium of Child Justice Cases) pamoja ripoti ya tathmini ya mafunzo kwa wadau wa haki za watoto (report on the impact assessment of trainings to juvenile justice frontline workers).

Jaji mkuu wa Tanzania. Mhe. Prof. Juma ametoa pongezi hizo kwenye uzinduzi wa kitabu hicho uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, leo Julai 19, 2021. Kitabu hicho kilichoandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kupitia ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya mtoto (UNICEF).

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Jaji Prof. Juma amezitaka mamlaka zinazosimamia na kutetea haki za mtoto kufanya kazi kwa kushikiana pamoja na kushiriki katika mafunzo mbalimbali yanayohusu mada za uendeshaji ya mashauri ya mtoto ili kuweza kuboresha mfumo wa ufatiliaji madai ya haki za mtoto kwa kushirikiana na mahakama nchini.

Mhe. Jaji Prof. Juma aliendelea kwa kusema kuwa wadau wa haki ya mtoto wanapaswa kushilikiana katika kutoa kipaumbele kwa masilahi ya haki za mtoto. Profesa IBrahimu amesema kuwa haki ya ulinzi pamoja na ustawi wa mtoto hauwezi kupatikana kwa kuiachia chombo cha mahakama peke yake bali inapatikana katika mfumo jumuishi wa haki ya mtoto ambao ni kivuli katika kuhakikisha usitawi na maendeleo ya mtoto,

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Prof. Juma alitoa wito kwa Waheshimiwa Majaji Wafawidhi wa kanda zote nchini, Mahakimu Wafawidhi wa Mikoa na Mahakama za Wilaya kuhakikisha kuwa wanapata nakala za kitabu hicho katika ofisi zao kwa ajili ya matumizi yao ili kusaidia kufanya rejea inapotakiwa kufanya hivyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Dkt. Paul Kihwelo Jaji wa Mahakama ya Rufani amesema kwa kushirikiana na Mahakama kuu ya Tanzania chini ya ufadhili wa Shirika la kuhudumia watoto dunia UNICEF uongozi wa chuo umekuwa ukiendesha mafunzo mbalimbali yanayohusu namna bora ya usimamizi wa kesi za mtoto mahakamani. 

 Mhe. Dkt. Kihwelo amesema kuwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama kimekuwa kikifanya tathimini katika kanda zote za mahaka kuu ili kuhakisha wadau mbalimbali walioshiriki kwenye mafunzo ya haki za mtoto wanaendelea kuwa na uelewa mkubwa katika kujuwa namna ya kusimamia kesi za madai kwa watoto mahakamani.

Mhe. Dkt Kihwelo aliendelea kwa kusema kuwa, hata hivyo kitabu cha mkusanyiko wa kesi za watoto kimetayalishwa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa maamuzi mengi ya mahakama za juu kuhusu haki za watoto kwa maafisa wa mahakama pamoja wadau wa wengine wa haki za mtoto ili kuweza kuongeza uelewa wa maamuzi mbalimbali yanayohusu haki ya mtoto mahakamani kupitia sheria ya mtoto ya mwaka 2009.

Akitaja faida kadhaa za kitabu hicho, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa kitabu hiki kinakumbusha kuwa, zipo sheria nyingi zaidi ya Sheria ya Mtoto ya 2009 [Law of the Child Act Na. 21 ya 2009], na kuwa Haki Mtoto haipatikani ndani ya Sheria moja tu bali kuna vifungu vya Katiba, Sheria mbalimbali, Kanuni, Taratibu, Mazoea na vigezo vingi ambazo kwa pamoja vinaleta mtirirko wa kufahamu mapana na marefu ya Haki ya Mtoto.


Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaohudumia Watoto (UNICEF), Bi. Sampathi Perera alitoa pongezi nyingi kwa Mahakama ya Tanzania na Chuo cha Uongozi wa Mahakama kwa kufanikiwa kuzindua kitabu hicho na kueleza kwamba uzinduzi wa kitabu hiki mafanikio makubwa sana kwani itawawezesha Majaji na Mahakimu kuendelea kutoa maamuzi sahihi kuhusu mashauri ya Watoto.

Uzinduzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) 2018/2019-2022/2023 wa kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya sheria nchini.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya Sheria nchini wanaohusika na haki za mtoto wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu wa ngazi mbalimbali, Wawakilishi wa Taasisi za Serikali, Wawakilishi kutoka Mashirika yasiyo ya Serikali na Wawakilishi wa UNICEF.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
أحدث أقدم