Na Dotto Kwilasa, DODOMA.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuona haja ya kuangalia namna ya kufanya mapitio upya ya Sera na sheria za kodi ili kuliweka vyema jambo hilo na kuondoa mkanganyiko unaojitokeza kwa jamii.
Hatua imekuja baada ya uamuzi wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wa kutaka tozo za miamala ya simu kuangaliwa upya na kuweka unafuu kwa wananchi.
Katibu wa Itikadi siasa na Uenezi (CCM) Shaka Hamdu Shaka amesema hayo wakati akiongea na Vyombo vya habari Jijini hapa ambapo amesema kwa mara nyingine Rais Samia amedhihirisha hekima, usikivu wake, uzalendo, umakini katika utendaji wake.
Akiongea katika Mkutano huo Shaka amesema,"Lakini zaidi Mama amedhihirisha kwa namna ambavyo amekuwa akiguswa moja kwa moja na changamoto za Watanzania na haki hii ni kielelezo tosha kuwa huyu ni Rais wa watu lakini na nao watu wana rais wao ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan,”.
Pamoja na mambo mengine amezitaka pia Serikali ya Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wa utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia kuona namna gani zitafanya mapitio ya sera, sheria za kodi ili kuliweka vyema jambo hili katika utekelezaji wake.
Katika hatua nyingine Shaka amezungumzia kuhusu ushindi kwenye jimbo la Konde,na kusema "Ni faraja iliyoje, namna gani mgombea wa CCM katika jimbo la Konde alivyoweza kukubalika na makundi yote,hii ni kwa sababu wananchi Wana imani na Serikali iliyopo madarakanai,"amesema na kuongeza;.
“Kwa niaba ya chama niwahakikishie kuwa hawatajuta juu ya uamuzi wao wa kukipa ushindi chama cha Mapinduzi, wamekikopesha chama Imani na tutalipa Imani katika kuwaletea maendeleo endelevu,”amesema.
Aidha amesema kuwa chama kimekuwa mstari wa mbele katika kuwasimamia viongozi katika ngazi zote ili kuhakikisha kuwa wanatimiza dhamira na matakwa ya wananchi katika kuwaletea maendeleo.
Kadhalika ,Katibu huyo Mwenzezi wa CCM amegusia malalamiko ya ACT Wazalendo ya kuchezewa rafu katika uchaguzi huo ambapo amesema vyama vya upinzani vimejisahau kwa kuhamishia siasa zao katika mitandao, matusi na kejeli na kusahau kuwa Watanzania wanataka maendeleo na si vinginevyo.
"Matusi hayawasaidii wananchi,wananchi wameelimika ,na hii imeonuesha dhahiri kwenye uchaguzi huo kuwa ni namna gani Watanzania na wapemba wameamka katika kujua ipi nyeupe na nyekundu katika kusimamia suala la maendeleo,"amesisitiza Shaka