Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Dkt. Mollel Atoa Onyo Kwa Watumishi Wanaotoka Kazini Muda Wa Kazi Na Kwenda Kufanya Kazi Binafsi


 Na WAMJW, DODOMA
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa onyo kwa watumishi wa sekta ya afya wanaotoka kazini muda wa kazi na kwenda kufanya kazi binafsi.

Dkt. Mollel amesema hayo jana mara baada ya kufanya kikao kazi na mameneja wa Mikoa toka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya nchini NHIF leo Jijini Dodoma.

“Waziri wa Afya aliunda timu na ikaonyesha jinsi ambavyo kuna ubadhirifu mkubwa kwenye eneo la dawa, kuna madaktari hawakai wakati wa kazi, dawa zinaibiwa na kukosesha huduma kwa wananchi na kuikosesha Serikali mapato” amesema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel ameonyesha kushangazwa na viongozi ndani ya maeneo husika kushindwa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wenye tabia hizo huku akisisitiza watumishi wenye tabia hizo kujirekebisha kabla ya yeye kuanza kuchukua hatua za kisheria.

“Kila mtu acheze kwenye namba yake sasa, usipocheza kwenye namba yako imekula kwako, usifikiri usipocheza kwenye namba yako itamhusu yule aliyefanya kosa, itakuhusu na wewe ambaye ulitakiwa uone” Amesema kwa lugha ya mafumbo akimaanisha kila mtumishi atimize wajibu wake kwenye nafasi yake pamoja na viongozi kuchukua hatua mapema.

Aidha Dkt. Mollel amesema kuwa amepanga kukutana wa wasajili wa vituo binafsi kuzungumza nao jinsi ya kuweka mipango endelevu ya kutumia wataalam waliopo katika sekta ya afya.

Dkt. Mollel ametoa onyo pia kwa wamiliki wa vituo binafsi vya kutolea huduma za afya nchini kuhakikisha wanafuata taratibu zote walizopewa kwenye usajili wa vituo hivyo na kuacha kutumia watumishi wa umma kinyume na taratibu za muda wa kazi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com