Na Dotto Kwilasa, DODOMA.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Kenani Kihongosi amewaagiza Wenyeviti na makatibu wa Chama hicho kwa ngazi ya mikoa kuanzisha utaratibu wa Club za mazoezi kwa kila Mkoa ili kuwahamasisha vijana kufanya mazoezi ili kuimarisha afya.
Ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Vijana Joging Club uliofanyika kwa lengo la kuwapa fursa vijana kuwa na utayari wa kufanya mazoezi mara kwa mara kuepukana na maradhi hasa ya Corona.
Akiongea kwenye uzinduzi huo Kihongosi amesema Jumuiya hiyo imezindua program hiyo ambayo itawahusu vijana kwa nchi nzima na sio Dodoma peke yake huku ikiongozwa na kauli mbiu ya"amani yetu,maisha yetu".
"Fanyeni mazoezi mjikinge na magonjwa,hasa katika kipindi hiki ambapo dunia inapambana na corona,"amesema.
Mbali na hayo Katibu huyo pia ametumia nafasi hiyo kuwashawishi watanzania hususani vijana,kuona umuhimu wa kuungana na Serikali Katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona kwa kukubali kupokea chanjo ya ugonjwa huo ambayo tayari imeshaingia nchini.
"Sisi kama vijana tunampongeza Mama yetu Samia kuleta suala la chanjo kwenye nchi yetu kwani linatuhakikishia usalama wa afya zetu hivyo ni wajibu wetu kujitokeza na kuepuka kusikil8za watu wanaopotosha,"amesisitiza.
Kupitia uzinduzi huo Katibu huyo wa jumuiya ya Vijana wa CCM amefikisha ujumbe pia kwa watanzania kuepukana na maneno ya kuyumbishwa kwani yanaweza kuvuruga amani ya nchi .
"Nchi yetu itajengwa na sisi watanzania,kumbukeni amani yetu ndiyo maisha yetu,amani ikitoweka ni sisi tunaotaabika,"amesema.
Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde amewahakikishia kuwapa ushirikiano vijana kwenye masuala ya michezo.
"Michezo ni ajira,ni matumaini yangu jumuiya hii ya UVCCM itaendelea kuwaandaa vijana ,nami naahidi kushirikiana na Katibu wa UVCCM kuunga mkono juhudi za Rais wetu Samia Suluhu Hassan tukiwa bega kwa bega kuhakikisha vijana wetu wanakuwa mstari wa mbele Katika kutetea na kulinda afya zao,"amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa Bill Chidabwa ameeleza kuwa michezo ni fursa kwa vijana kwani huwakutanisha, kuwaunganisha na kuwapa ajira.