Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Mabula Atatua Mgogoro Wa Mpaka Kati Ya Newala Na Masasi


 Na Munir Shemweta, MTWARA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amemaliza utata wa muda mrefu kuhusiana na mgogoro wa mpaka kati ya wilaya ya Masasi na Newala mkoani Mtwara baada ya kubainisha mpaka halisi baina ya pande hizo mbili.

Akiwa ameambatana na wataalamu wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Mtwara, Wakuu wa wilaya za Masasi na Newala, Wabunge pamoja na Wakurugenzi wa halmashauri zinazopakana ikiwa ni utelelezaji wa maagizo ya Makamu wa Rais Dkt Philip Isdor Mpango, Dkt Mabula alibainisha mpaka halisi uliopo kati ya kijiji cha Njenga na Miyuyu ikiwa ni takriban kilometa tano kutoka ulipoainishwa mpaka wa awali.

Akizungumza wakati wa usuluhishi wa mgogoro huo Julai 28, 2021 Naibu Waziri Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula alisema, jambo kubwa lililotatiza kwenye  mgogoro huo wa mpaka ni uhitaji wa maeneo ya kiutawala ambapo upande wa wakuu wa wilaya alisema hawakuwa na tatizo.

‘’Jambo linalotatiza sisi wengine ni katika suala zima ni sisi wachaguliwa kutaka maeneo ya kiutawala na wakuu wa wilaya wanasema hawana matatizo na ndiyo watawala sisi wachaguliwa hatutakiwi kuingia kabisa kwenye migogoro’’ alisema Dkt Mabula

Dkt Mabula aliongeza kuwa, iwapo kuna tatizo la kiutendaji kwenye eneo hilo basi wakuu wa wilaya wa maeneo husika wanaweza kushughulikia lakini kwa shida ya mipaka ya kiutawala  basi wakurugenzi wa halmashauri wana mamlaka ya kukubalina kwa kuwa suala hilo  linaangukia TAMISEMI na kusisitiza kwamba halmashauri zikikubaliana kazi ya wizara ya ardhi ni kubainisha mipaka.

Aliwaagiza Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya za Masasi na Newala mkoani Mtwara kwenda kwa wananchi wa vijiji vyenye migogoro kwa ajili ya kuzungumza na kuwapa elimu wakati kwa sasa mpaka unaotambuliwa ukiwa ni ule alioanishwa na yeye kulingana na vipo vya kitaalamu vinavyoonesha.

‘’Kama kuna maelezo mengine kuhusiana na mpaka huu wa Newala na Masasi basi itabidi watendaji na viongozi wa maeneo husika wakae pamoja na kushughulikia mgogoro huo ikiwa ni pamoja na kwenda uwandani, lengo ni kijiridhisha maana huwezi kupata suluhu ukiwa ofisini na mtkachokubaliana Wizara itakwenda kuweka alama za mipaka.

Diwani wa Kata ya Chilangala mkoani Mtwara Jamali Jafu aliutetea mpaka wa awali kati ya wilaya hizo mbili kwa kusema mpaka huo unapaswa kubaki eneo la Miyuyu  kwa kuwa ni mpaka wa asili tangu mababu kabla ya kuzaliwa wilaya ya Masasi.

Mkuu wa wilaya ya Masasi Claudia Kitta alisema, baada ya kuanishwa kwa mpaka huo kwa kuhusisha wataalamu wa pande zote sasa mpaka unaotambuliwa ubaki ulioanishwa na Naibu Waziri wa Ardhi na iwekwe alama katika eneo lililotambuliwa huku suala la vijiji vilivyoingia eneo lingine likifanyiwa kazi.

‘’Tukubaliane mipaka ni sahihi na vipimo vinaonesha na hili linguine la vijiji basi tutaangalia kijiji gani kimeingia huku au kimeingia kule na hili si tatizo kwa kuwa kinajitambua na huduma za jamii hazina mipaka’’ alisema Mkuu wa Wilaya ya Masasi Claudia Kitta

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Newala Alhaji Rajabu Kundya alisema, suala muhimu katika mgogoro huo ni kumaliza migogoro iliyopo kwenye vijiji vya mpaka na kueleza kuwa hatua hiyo itaoongoza maeneo ya uwajibikaji na kuonesha mpaka halisi wa wilaya na wilaya.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com