MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama chama Mapinduzi Mkoa wa Njombe (UWT) Scolastica Kevela amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa utendaji wake wa siku 100 madarakani ulionyesha mabadiriko makubwa kwa Tanzania.
Akizungumza Dar es Salaam Mama Kevela alisema kwa kipindi hicho cha siku 100, Rais Samia amefanya mambo makubwa ikiwemo kukutana na makundi mbalimbali ya wazee, wanawake, vijana na kurejesha mahusiano mengi ya kidiplomasia kiasi cha mataifa mengi kupongeza uongozi wake.
"Ameonyesha kweli nini maana halisi ya uongozi kwa kujali maslahi mapana ya wananchi wake na Taifa hili kwa ujumla huku akifungua fursa nyingi za uwekezaji kwa watu wote wenye nia ya kutaka kuja na kufanya uwekezaji wao nchini", alisema Mama Kevela
Alisema katika kipindi hicho Rais Samia amewatoa gizani watu wengi waliokuwa na changamoto za kimahakama ambapo kwa muda mrefu mashauri yao yalikuwa na changamoto mbalimbali.
Mbali na hilo Mwenyekiti huyo wa UWT alisema ndani ya uongozi huo wa siku 100 madarakani za Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha kuwa na imani yake kubwa kwa vijana kupitia uteuzi alioufanya hivi karibuni kwa wakuu wa Wilaya mbalimbali.
"Uteuzi wake umegusa makundi ya vijana kutoka maeneo mbalimbali jambo lilionyesha kuwa anawaamini katika utendaji wao wa kazi, hili limewafanya watu wengi kuzidi kumuunga mkono", aliongeza Kevela
Aidha alisema hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuunda tume maalumu ya kufuatilia mwenendo wa ugonjwa wa Covid 19, imeonyesha wazi nia ya kuifanya Tanzania kuungana na mataifa mengine katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo baada ya kipindi kirefu kuwa kama kisiwa kilichokuwa kimejitenga katika mapambano hayo.
Alisema kwa kipindi hicho cha siku 100 za uongozi wake, watanzania wengi wamejenga imani naye na kujawa na matumaini kuwa ataliwezesha taifa kupiga hatua kubwa kimaendeleo huku akiwataka watanzania kumuombea afya njema.
Social Plugin