AWLN KWA KUSHIRIKIANA NA TAASISI YA MWALIMU NYERERE ZAPEWA CHANGAMOTO YA KUSIMAMIA AMANI AFRIKA
Tuesday, July 27, 2021
Na Mwandishi wetu, Dar
Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere umepewa changamoto ya kukuza na kusimamia masuala ya umoja na amani katika Bara la Afrika ili kuleta maendeleo ya watu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ametoa wito huo wakati alipokutana na Mtandao huo pamoja na Taasisi ya Mwalimu Nyerere ikishirikiana na Shirika la Kimataifa la kutetea Haki na Maendeleo ya Wanawake (UN Women) leo jijini Dar es Salaam
“Agenda yetu ni muhimu, hamuwezi kusema kuwa tuna maendeleo kama hakuna amani…….amani ni sehemu ya Diplomasia ya Uchumi, kama amani huwezi kuitafuta kwa njia nyingine tuseme amani ni maendeleo na maendeleo ni amani,” Amesema Balozi Mulamula
Balozi Mulamula ameongeza kuwa, kwa kuzingatia kwamba amani ni matokeo ya haki juhudi zinahitajika katika kuhamasisha na kuunga mkono ushiriki kamili wa wanawake kama wadau muhimu wa kulinda na kutetea amani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku amesema kuwa Taasisi yake ina jukumu la kuhakikisha kuwa amani na haki zinapatikana hasa katika ukanda wa Maziwa Makuu.
“Tumepokea changamoto tuliyopewa na Mhe. Waziri na mimi ninakubaliana na yeye kabisa kuwa tushirikiane na wanawake katika kuhamasisha na kutunza amani na haki hasa kwa kushirikiana na wanawake ambao wamekuwa na mchango mkubwa sana wa kutunza amani na kuwa hakuna mpaka na yote yanawezekana,” Amesema Bw. Butiku.
Mtandao wa Uongozi wa Wanawake Afrika (AWLN) na UN Women umekuwa ukishirikiana katika kuisaidia Tanzania kuandaa Mpango kazi wa Kitaifa wa Utekelezaji wa ajenda ya wanawake, amani na usalama ya Maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Na. 1325
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin