Na Faraja Mpina, DODOMA
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amepiga marufuku tabia ya baadhi ya watendaji wa makampuni ya simu wasio waaminifu pamoja na washirika wao kuwarubuni wananchi kuuza maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano bila wao kujua kuwa wanauza kwa ajili ya ujenzi huo
Akiwa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Dodoma katika Wilaya ya Kongwa Mhandisi Kundo amesema kuwa kuna malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kurubuniwa kuuza maeneo yao lakini baada ya muda mfupi minara ya mawasiliano inajengwa katika maeneo hayo ambapo kodi ya ardhi ya eneo husika inaanza kulipwa kwa mmiliki mpya na mwananchi aliyeuza eneo lake kwa gharama ndogo hapati chochote
Ameongeza kuwa inafahamika kuwa kila mtu ana haki ya kisheria ya kumiliki eneo, kuuza na kupangisha eneo lake kwa kodi atakayoona inafaa lakini kinachofanyika katika baadhi ya maeneo ni wananchi kushawishiwa kuuza maeneo yao bila kujua kuwa ni eneo linalokuja kufanyiwa uwekezaji baada ya kufanyiwa utafiti na kuonekana linafaa kujengwa mnara wa mawasiliano
“Jukumu la Serikali ni kulinda maslahi ya wananchi hivyo naelekeza kila Mkurugenzi wa Halmashauri anapaswa kutambua umiliki wa eneo husika kabla ya kutoa kibali cha ujenzi wa mnara wowote ili kujiridhisha kama mmiliki wa eneo hilo anatambuliwa na Serikali ya kijiji husika”, alizungumza Mhandisi Kundo
Kwa upande wa malipo ya kodi ya ardhi kwenye maeneo yanayoenda kujengwa minara Mhandisi Kundo ameelekeza mikataba yote kufanyika kupitia ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kwasababu yeye ndiye mwenye wataalam wanaojua thamani na gharama za maeneo yaliyopo ndani ya halmashauri husika
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remedius Mwema Emmanuel amesema kuwa katika Wilaya ya Kongwa kumekuwa na malalamiko mengi na migogoro kutoka kwa wananchi kuhusu kurubuniwa kuuza maeneo yao na wakati mwingine wenyeviti wa vijiji wamekuwa wakitumika kuhamasisha wananchi
Ameongeza kuwa katika kata ya Nghumbi kijiji cha Mbagirwa kuna mnara wa mawasiliano lakini mmiliki wa eneo husika hajulikani na Serikali ya kijiji haipati kodi yeyote kutoka katika mnara huo
Aidha, katika ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma Naibu Waziri huyo ameendelea kupokea na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazogusa Sekta ya Mawasiliano ikiwa ni pamoja na kupokea mahitaji ya wananchi ya kuboreshewa huduma ya mawasiliano ya simu na intaneti
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari