Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameiagiza Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) kuhakikisha inadhibiti ushiriki wa Watoto chini ya miaka 18 katika michezo ya kubahatisha na kuandaa mkakati na mapendekezo kwa Serikali ya namna ya udhibiti huo kutokana na athari zake katika jamii.
Mhandisi Masauni ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam alipotembelea na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Bodi hiyo pamoja na wafanyakazi, katika mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.
“Katika eneo hili ya ushiriki wa Watoto katika michezo ya kubahatisha niseme kwamba kama wasimamizi mliopewa jukumu la kudhibiti Watoto kushiriki michezo hiyo hamjafanya kwa viwango vya kutosha na sijaona maelezo ya kimkakati ya kuridhisha”, alieleza Mhandisi Masauni.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Bw. James Mbalwe, alisema kuwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanzia 2016/17 hadi 2020/21 jumla ya kodi zilizokusanywa na Bodi hiyo ikiwa ni mapato ghafi yanayotokana na michezo ya kubahatisha yalifikia shilingi bilioni 428.97, bila kuhusisha kodi nyingine ikiwemo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Alisema kuwa dhima ya Bodi hiyo ni kukuza, kusimamia, kufuatilia na kudhibiti tasnia ya michezo ya kubahatisha nchini ili kuhakikisha uadilifu, kuongeza faida za muda mrefu za kijamii na kiuchumi na ulinzi wa umma kwa kutekeleza Sheria yenye viwango vya kimataifa na mazoea bora.
Alisema kuwa Michezo ya kubahatisha nchini imeajiri zaidi ya watu 20,000 na kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021, michezo hiyo imewezesha kuwepo kwa mzunguko wa fedha katika sekta ya michezo ya kubahatisha unaofikia zaidi ya shilingi trilioni 3.2 na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Mafanikio mengine ya Bodi ni kutokutegemea ruzuku ya Serikali katika kujiendesha ambapo tunajiendesha kwa faida na katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2018/2019 hadi 2020/2021, GBT ilifanikiwa kukusanya mapato kiasi cha shilingi bilioni 30 na katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 taasisi yake inatarajia kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 14.3.” aliongeza, Bw. Mbalwe.
Aidha, alisema kuwa Taasisi yake inachangia Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo mwaka 2020/2021 walichangia shilingi bilioni 3.05 na kwamba azma ya GBT ni kuendelea kuchangia katika mfuko huo kwa mujibu wa Sheria na miongozo inayotolewa na Serikali.
Kuhusu Watoto wasiokidhi vigezo vya kushiriki katika michezo ya kubahatisha, Bw. Mbalwe, alimshukuru Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Yusuph Masauni kwa kuibua changamoto mbalimbali ikiwemo ya Watoto chini ya miaka 18 kushiriki katika michezo ya kubahatisha, jambo aliloahidi kuwa atalifanyia kazi ili kujenga jamii bora kwa manufaa ya baadae ya maendeleo na ustawi wa Taifa.