Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NIDA TEXTILE INDUSTRIES YAKUMBANA NA RUNGU LA WAZIRI JAFO, WAPEWA SIKU 45


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Selemani Jafo ametoa siku 45 kwa Kiwanda cha kutengeneza nguo cha NIDA  Textile Industries kuhakikisha kimepata kibali cha kutiririsha maji ambayo yanaingia katika  Mto ulioko katika eneo hilo,  kutoka katika Mamlaka ya Bonde  Mto Wami- Ruvu kinachothibitisha ubora wa maji wanayotiririsha ni salama kwa Mazingira  na hayana athari yoyote kwa mazingira.

Ametoa agizo hilo Mkoani Dar es Salaam  alipotembelea kiwanda hiko kilichopo  katika eneo la Tabata katika Manispaa ya Ubungo alipokua katika ziara yake ya siku moja na kubaini hakuna  kibali cha kutiririsha maji ambacho  ni muhimu kwa sababu Kiwanda hiko kina mfumo wa kutiririsha maji taka kwahiyo kinatakiwa kuwa na kibali hiko .

“Ninatoa siku 45 ikiwa na maana ya mwezi mmoja na nusu muwe mmeshapata kibali kutoka Mamlaka ya Bonde  kuhusiana na maji taka mnayotiririsha kama ni salama au la mana maji haya hayaonyeshi kwa macho maji haya ni salama kwa mazingira  na  viumbe hai” Waziri Jafo

Aidha Waziri Jafo alitembelea kiwanda cha kutengeneza sabuni cha Royal Soap and Detergents kilichopo Kata ya Mabibo katika Manispaa ya Ubungo   kujionea changamoto za  uchafuzi wa mazingira katika eneo hilo ambazo zimekua zikilalamikiwa kwa muda mrefu na Wananchi wa eneo hilo la Kata ya Mabibo ikiwemo hewa chafu inayotoka kiwandani hapo .

Akiwa Kiwandani hapo alisikiliza pande zote yani Upande wa Kiwanda na Wananchi ambapo waliwakilishwa na Diwani wa Kata hiyo Mh. Joseph Kleruu na hatimaye alitoa maagizo kuwa ameona kuna changamoto ya Kimahusiano kati ya Wananchi wa eneo hilo na mwenye Kiwanda hivyo ameagiza kifanyike kikao kati ya mwenye Kiwanda, Afisa Mazingira wa Manispaa pamoja Diwani na Mwenyekiti wa Mtaa huo  ambao ni Wawakilishi wa Wananchi kwa pamoja wafikie makubaliano halafu taarifa ya Makubaliano hayo iende kwa Mkuu wa Wilaya ya Manispaa ya Ubungo .

‘Nimeona kuna changamoto ya kimahusiano katika eneo hili tafadhali wekeni mahusiano mazuri na Wananchi wanaowazunguka hiyo ni muhimu sana naagiza mfanye kikao ndani ya wiki mbili kupata ufumbuzi wa suala hili na ndani ya miezi sita tutakuja tena kujionea katika suala la mazingira utekelezaji wa makubaliano hayo umefanyika au la ” Waziri Jafo

Akiongea baada ya kupokea maagizo hayo Mkuu wa Wilaya Manispaa  ya Ubungo Mh. Kheri James  alimuhahikishia Waziri Jafo kupokea maagizo hayo na atayafanyia kazi na taarifa ya makubaliano itapelekwa Ofisini kwa Waziri kama alivyoagiza.

Naye Meneja wa Uendeshaji wa Kiwanda hiko Ntula Shalanda amemuahidi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Selemani Jafo kupokea maagizo hayo na kuyafanyia kazi na watakutana na Wawakilishi hao wa Wananchi kama alivyoagiza.

Katika ziara hiyo Waziri Jafo aliambatana na Mkuu wa Wilaya wa Manispaa ya Ubungo Kheri James pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Manispaa ya Ubungo na Wataalamu wa Mazingira kutoka NEMC na Manispaa ya Ubungo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com