Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba akitoka katika hospitali ya Sali International iliyopo mkoani Dar es Salaam leo mara baada ya kupata chanjo.
**
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba amepata chanjo ya kwanza ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya COVID-19 katika Hospitali ya Sali International iliyopo mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kupata chanjo hiyo aina ya AstraZeneca, Prof. Lipumba amesema kuna umuhimu kwa Watanzania wengi kupata chanjo hiyo ya hiari ili kujikinga na janga hilo linalosumbua ulimwenguni na taifa la Tanzania kwa ujumla.
“Nakumbuka Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na Mwakilishi wa Mfalme wa Abu Dhabi kuhusu upatikanaji wa chanjo, naamini Serikali yetu itatumia fursa hiyo ya kupata chanjo kwa msaada wa nchi hizo”, amesema Prof. Lipumba.
Ametoa wito kwa Serikali ya Tanzania kukubali chanjo hizo zilizopitishwa na kukubaliwa na Jumuiya za Umoja wa Mataifa sambamba na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kutokana na usalama wake kwa Wananchi.
“Mimi binafsi nimepata fursa hii kutokana na Mke wangu kufanya kazi katika Umoja wa Mataifa (UN), Bangladesh katika Shirika la UNICEF, wao wanatakiwa kupata chanjo na Familia zao hivyo nililetewa Fomu ya kujaza ili kupata chanjo hii katika Hospitali hii ya Sali International hapa Dar es Salaam.” ameeleza Prof. Lipumba.
“Nashauri pia kwa Serikali kutoa mafunzo na Elimu kwa Wahudumu wa Afya na Wananchi kwa ujumla kuhusu kujikinga na janga hili sambamba na matumizi ya chanjo hiyo ya hiari.”
Social Plugin