Na Prisca Ulomi, WMTH
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Serikali itahakikisha mawasiliano ya utangazaji yanafika kote nchini kwa kuwa mawasiliano ya redio yanawapata taarifa mbali mbali wananchi na Wizara tunapenda kuona maudhui ambayo yanaendana na utamaduni wetu Tanzania na yanajibu changamoto za wananchi kwa kuwa sasa kuna taarifa ambazo sio sahihi zinatolewa kwa wananchi kupitia baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Ameongeza kuwa Serikali itapunguza gharama za leseni za redio jamii na za pembezoni zilizopo ngazi ya Wilaya ili kuondoa adha ya wananchi waishio pembezoni mwa mipaka ya nchi yetu kwa kusikiliza redio za nchi nyingine za jirani
Dkt. Ndugulile ameyasema hayo jana akiwa Mgeni Rasmi kwenye uzinduzi na makabidhiano ya studio ya kisasa ya kidijitali ya TBC ya redio jamii ya Mjini Dodoma kwa kuwa ukarabati, ununuzi na ufungaji wa mitambo ya studio hiyo umegharamiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambayo ni moja ya taasisi zilizo chini ya Wizara hii. Aidha, ameahidi kuwa Wizara itaangalia namna ya kushirikiana na Shirika la utangazaji Tanzania (TBC) kuwezesha upatikanaji wa njia maalumu na kifaa cha satelaiti cha kutunza na kuhifadhi taarifa za studio hiyo
Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ameishukuru Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuwezesha ukarabati na kufunga mitambo mipya ya studio ya redio jamii ya TBC iliyopo Dodoma ambayo itasikika kwenye mkoa wa Dodoma, Singida, Iringa na maeneo ya jirani kwa kuwa moja ya kipaumbele cha Wizara ya Habari ni kuiwezesha TBC kifedha, mtaji na kuendeleza wataalam.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Stanslaus Nyongo amesema kuwa Kamati imeridhishwa na studio hii mpya ya TBC kwa kuwa Bunge limekuwa na nia hii na leo limetimia ili wananchi wapate taarifa za Serikali kwa kuwa vyombo vya habari vipo vingi ila TBC ni chombo cha uhakika na wananchi wanapenda kusikiliza taarifa kutoka TBC
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Antony Mtaka amesema kuwa redio ya jamii ni nzuri ili wananchi wa eneo husika wapate taarifa zinazowahusu na watahakikisha taasisi za Serikali za Mkoa wa Dodoma zitatumia studio hii kutangaza taarifa zao kwa wananchi mathalani masuala ya maji, umeme na kulipia matangazo ili studio iweze kujiendesha
Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema kuwa taasisi yake imetoa shilingi bilioni 1.07 kukarabati, kununua na kufunga mitambo ya studio hiyo ambapo mwakilishi wa Bodi ya UCSAF, Mhandisi Francis Mihayo ameiomba bodi ya TBC kuhakikisha mitambo iliyonunuliwa inatunzwa na kutumika kuendana na thamani ya fedha iliyonunulia
Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba amesema kuwa TBC wametoa shilingi milioni 163 kukarabati studio hiyo na imeunganishwa na redio nyingine ya TBC Taifa na TBC FM na kufafanua kuwa huu ni mwanzo wa kuendeleza Dodoma kimawasiliano kwa kuwa Dodoma ni Makao Makuu ya nchi na Serikali.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Social Plugin