Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YARUHUSU USHINDANI KWENYE MBOLEA


 Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mwanza
Kwa kuwa mfumo wa ununuzi wa pamoja umekuwa ukitumika kwa lengo la kupata mbolea kwa bei nafuu kutoka kwa wazalishaji na kwa kuwa mazingira ya sasa duniani yanaonesha kuwa mfumo wa ununuzi wa pamoja hauwezi kukidhi mahitaji hayo hivyo Wizara ya Kilimo imeamua kuruhusu ushindani li kila mwenye uwezo wa kuleta mbolea na kuiuza afanye hivyo ili mbolea iwepo nchini kwa wingi na bei shindani.

Uamuzi huo wa serikali kuruhusu kila mfanyabiashara kuagiza mbolea itaifanya Tanzania kuwa kitovu (HUB) cha mbolea kwa matumizi ya ndani na nchi zinazoizunguka.

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ametoa msimamo huo wa serikali  tarehe 4 Julai 2021 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati alipofanya ziara ya siku moja katika Ofisi za Bodi ya Pamba Jijini Mwanza.

Amesema kuwa kwa kuzingatia Kanuni ya 7(4) ya Kanuni za Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja Na. 49 za mwaka 2017, hivyo amewataka wafanyabiashara wote wenye nia ya kuingiza mbolea nchini kwamba, wako huru kufanya hivyo bila kupitia zabuni ya uagizaji wa mbolea kwa pamoja.

Waziri Mkenda amesema kuwa Katika kufanikisha mpango huo, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa ushindani unakuwa wa haki na Wizara ya Kilimo kwa muda wote itakuwa tayari kushirikiana na Kampuni yoyote itakayoagiza mbolea.

“Nitoe wito kwa wafanyabiashara wote wa mbolea kuwasilisha maombi yao ya kuagiza mbolea kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea haraka iwezekanavyo” Amekaririwa Prof Mkenda

Ndugu Wanahabari, nimewaita hapa ili  nizungumze nanyi kuhusu suala la upatikanaji wa mbolea nchini hususan kwa msimu wa 2021/2022.

Prof Mkenda amesema kuwa upatikanaji wa mbolea hapa nchini unategemea uzalishaji unaofanywa na viwanda vya ndani na upungufu hufidiwa kwa kuagiza nje ya nchi kupitia mfumo wa ununuzi wa pamoja (bulk procurement) na uingizaji unaofanywa na Kampuni za mbolea zinazopatiwa vibali na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).

Amesema kuwa mahitaji ya mbolea kwa msimu wa 2020/2021 yalifikia tani 718,051 na upatikanaji ulifikia asilimia 82 hadi mwezi Mei, 2021. Katika mazingira ya kawaida kipindi cha kati ya Julai na Oktoba kila mwaka watumiaji wakubwa wa mbolea duniani hupunguza matumizi ya mbolea na hivyo bei katika soko la dunia hupungua.

Kwa mwaka 2021 hali hiyo imekuwa tofauti na miaka mingine kwa kuwa bei za mbolea duniani zimeendelea kupanda kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo athari za Ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19) ambapo baadhi ya viwanda vimepunguza uzalishaji na kusababisha bei kupanda kutokana na kuwepo kwa mahitaji makubwa ikilinganishwa na upatikanaji hususan kwa nchi watumiaji wakubwa wa mbolea.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com