Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SUZA : NJOONI KWENYE BANDA LETU KWENYE MAONYESHO YA TCU



 Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimewakaribisha na kuwashauri  wananchi wakiwemo wazazi walezi kutembelea banda lao la Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia Vyuo Vikuu wapatiwe maelekezo sahihi ya kozi zitolewazo na chuo hicho ili waweze kuwashauri watoto wao taaluma bora za kusoma katika mwaka wa masomo wa 2021/22.

Aidha, chuo hicho kimewakaribisha wanafunzi waliomaliza kidato cha sita kufika katika banda lao ili wapatiwe maelekezo ya kufanya udahili kutoka kwa wataalamu na taaluma bora za kusoma zinazofundishwa na SUZA.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam  katika Viwanja vya Mnazi Mmoja kwenye uzinduzi wa maonesho hayo yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) na Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Masoko wa SUZA, Khadija Sadiq Mahumba.

Amesesma wazazi wataofika katika banda lao watapatiwa elimu bora ya namna ya kuchagua kozi zinazowafaa watoto huku akibainisha wanafunzi watapatiwa elimu bora ya namna ya kuchagua kozi zinazowafaa kwani chuo hicho kina mazingira bora ya kujisomea.

" Wanafunzi wahudhurie kwenye banda letu wasiwe na wasiwasi watapata elimu sahihi ya kufanya udahili mwaka wa  masomo wa 2021/22 hata wazazi tunawashauri watembelee hapa kuna wataalamu watawaelekeza kozi tulizonazo kwa manufaa ya watoto wao," amesema Khadija.

Amebainisha kuwa wanafunzi watakaojiunga na chuo hicho watapata fursa ya kusomea taaluma mbalmbali katika ngazi za Cheti, Astashahada, Shahada, Shahada ya Uzamili, Shahada ya Pili ya Uzamili.

Amesisitiza kuwa chuo hicho kinafundisha taaluma mbalimbali kwa nadharia na vitendo na kwamba wanafunzi wataokajiunga na taaluma za afya, udaktari pamoja na upasuaji wa meno watasoma kwa vitendo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo visiwani humo.

Alizitaja taaluma zinazofundishwa na SUZA  ni Kilimo, Ualimu,Utalii, Upasuaji wa meno, ufundishaji wa Lugha ya Kiswahili na za kigeni, usimamizi wa biashara, afya na udaktari, kompyuta, mawasiliano na uhandishi wa habari pamoja na ufamasia. 

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Udahili wa SUZA, Ali Shauri Jecha amesema katika udahili wa mwaka wa masomo wa 2021/22 chuo hicho kimejipanga kutoa sapoti ili kuhakikisha wanafunzi wanafanya udahili wa vyuo na kozi kwa usahihi.

Ali amesema watafanya matembezi katika shule lengo likiwa kuwafikia wanafunzi wajue kozi zitolewazo na SUZA  pamoja namna bora ya kufanya udahili kupitia mtandaoni na kwamba Zanzibar wametenga dawati maalum la kutoa elimu na udahili kwa wanafunzi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com